Fernandes akanusha kumkwaza Solskjaer

Porto, Ureno. Bruno Fernandes amekanusha taarifa kwamba alizozana na kocha wake, Ole Gunnar Solskjaer, lakini alikiri kukasirishwa na tukio la kutolewa dhidi ya Tottenham.

Kulikuwa na madai kwamba nyota huyo wa Manchester United aligombana na wachezaji wenzake kabla ya kutolewa wakati wa mapumziko, wakati timu yao ikichakazwa kwa mabao 6-1 na Tottenham.

Nyota huyo wa kimataifa wa Ureno, ambaye alikuwa na timu ya taifa kwa wiki mbili, alikuwa akijadiliwa juu ya kugombana na kocha raia wa Norway katika mwanzo mbaya wa timu hiyo.

Lakini alivunja ukimya na kusisitiza kuwa kocha wake yupo sahihi juu ya mbinu zake, akikanusha madai ya kwanza kuwa alitamka maneno ya kukosoa ufundishaji wake walipozibuliwa na Spurs.

Fernandes mwenye miaka 26, ambaye alisajiliwa Januari, aliiambia Sport TV ya Ureno: “Siku zote nina adabu kwa kocha wangu, kwasababu ndiye mtu pekee aliyenihitaji na kuniamini.

“Kuhusu mfumo anaoutumia uko sawa kwangu. Kocha aliamua kunitoa dhidi ya Spurs, lakini aliniambia kuwa mchezo ulishakuwa juu yetu na tuna mengi zaidi ya kufanya.

“Ni kweli kwamba sikufurahishwa na hilo la kutolewa baada ya dakika 45, lakini nilielewa. Sikuzungumza lolote baya la kufanya timu ijisikie vibaya.”