Ferland Mendy mrithi wa kudumu wa Mbrazili Marcelo pale Santiago Bernabeu

MADRID, HISPANIA. HATIMAYE Real Madrid imefanikiwa kuvunja benki kwa mara nyingine na kumchukua beki wa kushoto wa Lyon na Timu ya Taifa ya Ufaransa, Ferland Mendy kwa dau la Pauni 45 milioni.

Anakuwa mmoja kati ya wachezaji watano walionunuliwa na Real Madrid katika dirisha hili la uhamisho mpaka sasa. Kinatokea wapi hiki kipaji cha Kifaransa?

Azaliwa Ufaransa, asili ni Senegal

Jina lake ni Ferland Mendy na alizaliwa Juni 8, 1995 katika Kitongoji cha Meulan-en-Yvelines, Ufaransa huku wazazi wake wakiwa wahamiaji kutoka Senegal.

Awali Mendy alianzia soka katika Klabu ya PSG akicheza soka la vijana lakini aliachwa baada ya kuumia nyonga ambayo pia ilimlazimisha akose dili kubwa la soka akiwa na umri wa miaka 15. Ni nyakati hizo hizo pia alimpoteza baba yake mzazi.

Operesheni ya nyonga ilisababisha atembelee kiti cha wagonjwa huku madaktari wakimwambia asingeweza kucheza soka tena, lakini mwenyewe alikaririwa alikaa hospitalini kwa kipindi cha miezi sita hadi saba.

Baada ya kutoswa na PSG, akiwa na umri wa miaka 17, Mendy aliamua kujiunga na klabu ya ridhaa ya mtaani kwao ya FC Mantois 78. Ni hapo ndipo ilipoonekana kuwa bado angeweza kuwa mmoja kati ya wachezaji wazuri na mtu anayeitwa Johann Louvel, ambaye alikuwa akisimamia timu ya vijana la Le Havre aliamua kumfukuzia kwa karibu.

Baadaye alijiunga na Klabu ya Le Havre ambayo inashiriki Ligi Daraja la Pili Ufaransa. Ligi hiyo ni maarufu kwa kutoa mastaa wengi wakubwa wa soka wanaotamba sasa kama vile Paul Pogba, Lassana Diarra na Riyad Mahrez.

Maendeleo ya Mendy yamekuja kwa haraka kwa sababu mpaka kumalizika kwa msimu wa 2016–17 alikuwa ameichezea Le Havre mechi 12 tu katika Ligi Daraja la Pili na wakati huo alikuwa na umri wa miaka 21.

Katika msimu wake huo, kutokana na tabia yake ya kupanda mbele mara kwa mara alijikuta akipika mabao matano na kufunga mabao mawili. Mwisho wa msimu alitajwa katika kikosi cha kwanza League 2 cha msimu.

Msimu uliofuata baada ya kuuzwa kwa beki wa kushoto wa kimataifa wa Madagascar, Jerome Mombris, alionyesha kiwango cha uhakika akicheza mechi 38 huku mechi 37 akiwa ameanza. Kiwango chake kilisababisha klabu za Ligi Kuu ya England, West Brom, Brighton na Crystal Palace zimnyatie.

Atinga lyon, atangaza jina

Mendy alisaini mkataba wa miaka mitano katika Klabu ya Lyon huku Le Havre ikilipwa dau la Euro 5 milioni na kukiwa na ongezeko la Euro 1 milioni kutokana na kiwango ambacho angeonyesha kwa wababe hao katika michuano mbalimbali.

Uhamisho wake ulipigwa zengwe na baadhi ya mashabiki wa Lyon walioamini alikuwa mwepesi na angeshindwa mikikimikiki ya Ligi Kuu ya Ufaransa ambayo ina matumizi makubwa ya nguvu. Hata hivyo, katika msimu wake wa kwanza alifanikiwa kuwaziba midomo walioukosoa uhamisho wake.

Alicheza zaidi ya dakika 2,500 na katika mechi ambazo alicheza 16 hakuruhusu bao huku akipika mabao manne.

Msimu ulioisha Mendy alicheza mechi 45 na kati ya hizo alianza mechi 44 huku akifunga mabao matatu na kupika mabao matatu. Alicheza zaidi ya dakika 3,600. Kutokana na kiwango chake Klabu za Juventus, Barcelona na Real Madrid zilianza kumnyatia lakini ilikuwa ni Madrid chini ya Kocha wa Kifaransa, Zinedine Zidane iliyoamua kufanya kweli.

Aitwa kumng’oa Marcelo Madrid

Juni 12, 2019, Real Madrid ilitangaza kumnasa Mendy kwa dau la Pauni 47 milioni huku akisaini mkataba wa miaka sita. Kununuliwa kwake ni kiashiria kwamba Madrid imepata mtu sahihi wa kumrithi beki wake wa kimataifa wa Brazil, Marcelo.

Wakala wa Mendy, Yvan Le Mee ambaye ni mmoja kati ya mawakala wazoefu Ulaya anaamini Mendy ni ‘Kylian Mbappe wa ulinzi’ kutokana na kipaji chake maridhawa.

“Mendy ni Kylian Mbappe wa upande wa ulinzi wa kushoto. Tofauti na watu wanavyoamini, nafasi ya beki wa kushoto ni ngumu kuipata baada ya ile ya mshambuliaji kwa sababu ni ngumu kupata mabeki wa nafasi hiyo.”

“Mendy ni mzuri katika kushambulia na kukaba, kitu ambacho ni mara chache sana kukiona kwa wengine. Mabeki wanaoleta uwiano katika kwenda mbele na pia imara katika kurudi nyuma ni ngumu kuwapata. Katika umri wake hakuna kama yeye. Kando ya Andy Robertson, ambaye hawezi kuhama Liverpool na pia Lucas Fernandez ambaye ana timu yake, hauwezi kuwapata.”

Atamba Ufaransa, hajacheza vijana

Mendy ni mmoja kati ya wachezaji wachache kutoka katika mataifa makubwa kisoka ambao hawajawahi kuzichezea timu za vijana. Inatokana na ugonjwa wake akiwa kijana na alipokuwa fiti aliibukia timu ya wakubwa moja kwa moja.

Aliitwa katika kikosi cha wakubwa cha Ufaransa Novemba 2018 baada ya kuumia wajina wake, Benjamin Mendy wa Manchester City wakati kikosi cha Ufaransa kilipoitwa kwa ajili ya mechi dhidi ya Uholanzi na Uruguay.

Alicheza mechi yake ya kwanza dakika zote 90 dhidi ya Uruguay na kuanzia hapo ameanza kuichukua nafasi ya Benjamin kimyakimya ingawa wote wawili wanafanana kuanzia majina hadi staili zao za mchezo.