Ferdinand aukubali mziki wa Fabinho

Muktasari:

Kiasili Fabinho ni kiungo mkabaji lakini kutokana na kupata majeraha kwa  Virgil van Dijk kumemfanya kocha wa Liverpool, Jürgen Klopp  kumchezesha kama beki wa kati  sambamba na Joe Gomez.

AMSTERDAM, UHOLANZI. KIWANGO ambao amekionyesha kiungo wa Liverpool, Fabinho ambaye alicheza  nafasi ya Virgil van Dijk  kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya  Ajax, kimemkosha beki wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand.

Akiwa kama beki wa kati, Mbrazil huyo alionyesha kiwango cha juu ambacho  kiliisaidia Liverpool kuibuka na  ushindi wa bao 1-0 wakiwa ugenini.

Ferdinand ambaye alikuwa akiumbachua mchezo wa Ajax dhidi ya Liverpool  kwenye kituo cha BT Sport, amesema  Fabinho na Gomez wanaweza kuendelea  kukifanya kikosi cha Klopp kuwa salama kwenye idara yao ya ulinzi.

"Huyu jamaa ni kiongozi na alikuwa akicheza muda mwingine kama beki wa kulia wakati akiwa Monaco kwa hiyo ni mzuri kwenye kuzuia. Kilichopo ni kuendelea kuchezeshwa pamoja na Joe Gomez ili kuzoeana kama mabeki pacha.

"Tatizo limepatiwa ufumbuzi, anaweza kuvaa viatu vyake (van Dijk) na akacheza vizuri kwenye eneo hilo akiwa na Gomes ambaye naye ni miongoni mwa mabeki bora wa kati  kwa sasa.

"Nadhani baada ya wiki kuwa na majeruhi kwenye kikosi chake alafu unacheza ugenini na kupata pointi huku ukiwa hujaruhusu  bao ni kitu kizuri kwa Klopp, anaweza kujiona daktari," amesema.

Liverpool hawajaruhusu bao kwenye michezo minne kati ya mitano ya mwisho kucheza kwenye Ligi Kuu England huku Fabinho akitumika kwenye idadi hiyo kama beki wa kati.

Mchezaji mwenzake na Fabinho, James Milner amesema Mbrazil huyo amekuwa na mchango mkubwa katika matokeo ambayo wameyapata kwa kuokoa hatari ambayo kama angezembea basi wangeruhusu bao huko Amsterdam.

 

Ajax walikuwa kwneye nafasi ya kusawazisha, alikuwa ni Dusan Tadic ambaye alimshinda maarifa kipa wa Liverpool Adrian na kupiga mpira ambao ulikuwa ukiingia nyavuni lakini Fabinho aliondosha mpira ule.

"Ni mchezaji wa daraja la juu (Fabinho) na mchezaji wa daraja lake anaweza kuendana kwa haraka, amewahi kucheza kwenye eneo hilo, tumepata matokeo muhimu," amesema vetereni huyo.

Bao la Liverpool kwenye mchezo huo, alijifunga beki wa kushoto wa Ajax na timu ya taifa la Argentina,  Nicolas Tagliafico.