Fei Toto, Makapu na Abdul kuwakosa Singida

Tuesday July 14 2020

 

By THOMAS NG'ITU

KOCHA Luc Eymael wa Yanga amesema katika mchezo wao wa kesho dhidi ya Singida United atawakosa nyota wake Said Makapu na Feisal Salum ambao wana kadi za njano.

Makapu, Feisal na Juma Abdul wote wana kadi tatu za njano walizopata katika mechi zilizopita hivyo kuwafanya kukosa mchezo wa kesho.

Akizungumza kwa njia ya simu leo mchana, Luc alisema anabidi atulize akili kuhakikisha anatoka na matokeo katika mchezo huo licha ya kwamba katika mazoezi ya jana jioni (Jumatatu) wachezaji wengi hawakufika mazoezini huku kukiwa hakuna taarifa rasmi.

"Jana wewe mwenyewe uliona wachezaji waliokuwepo mazoezini, inabidi mazoezi ya leo niangalie nani na nani ambaye anakuja kisha ndio nijue naendaje dhidi ya Singida na tunatakiwa kushinda mchezo huu".

Luc aliongeza anatarajia kuona wachezaji wake Kelvin Yondani na Papy Tshishimbi leo wataenda uwanjani na kama wakienda inaweza ikawa rahisi kwake kupanga kikosi.

"Kelvin kama akija naweza nikamuweka katika nafasi ya beki wa kati sambamba na Lamine au nikamchezesha Sonso na Yondani kisha kwenye kiungo nitamuweka Makame na namba nane nitajua akija mwingine mazoezini, kukosekana kwa wachezaji jana inashtua," alisema.

Advertisement

Wachezaji ambao walicheza mchezo wa juzi na hawakuwepo mazoezini ni Papy Tshishimbi, Haruna Niyonzima, Metacha Mnata na Juma Abdul.

Wachezaji waliokuwepo katika mchezo wa juzi na kucheza dakika 90, Jaffary Mohamed, Feisal Salum, Lamine Moro, David Molinga na Deus Kaseke wao walikuwa wanafanya mazoezi ya kunyoosha viungo kwa pembeni.

Wachezaji wengine waliokuwa wanafata programu ya mwalimu kocha Luc Eymael kwenye mazoezi ya jana Jumatatu ni Faruk Shikhalo, Ramadhan Kabwili, Paul Godfrey, Tariq Seif, Ally Mtoni, Juma Mahadhi, Mrisho Ngassa, Yikpe Gnamien, Abdulaziz Makame, Mrisho Ngassa, Adeyum Saleh, Rafael Daud, Patrick Sibomana, Ditram Nchimbi na Eric Kabamba.

Advertisement