JICHO LA MWEWE: Februari 16 inapokuwa muhimu zaidi kuliko kesho

Monday February 11 2019

 

By Edo Kumwembe

MITANDAONI ambako siku hizi kunatoa taswira ya fikra zetu nadhani mechi ya Simba na Yanga imekuwa muhimu kuliko mechi ya Simba ya Al Ahly. Tarehe 16 bado mbali lakini mechi ya Al Ahly nilidhani ingebeba umuhimu kwa Simba.

Rafiki yangu mmoja wakati mechi ya Al Ahly na Simba ikiendelea pale Alexandria akili yake ilikuwa ni namna ambavyo Simba ingelipiza kisasi cha mabao hayo katika mechi ya Yanga. Wakati huo mechi ya Al Ahly na Simba ilikuwa mapumziko na wenyeji ilikuwa inaongoza mabao 5-0. Nilishangaa

Kilichonishangaza ni kwamba kijana aliyekuwa anaisubiri mechi ya Yanga kwa hamu kubwa kuliko alichokuwa anakiona Misri. Anatamani kuja kuiongoza Simba siku moja. Kumbe na yeye akipewa nafasi atakuwa wale wale tu.

Mpira wetu unashangaza lakini inabidi tuuvumilie. Baada ya mechi ile ambayo Simba ilikuwa imefungwa mabao 5-0 mpaka mwisho mjadala ulihamia katika mechi ya Simba na Yanga badala ya mechi ya marudiano ya kesho Jumanne.

Aliyeifufua mechi hii walau kidogo ni tajiri wa timu, Mohammed Dewji. Baada ya mkutano wake na waandishi wa habari Ijumaa iliyopita walau aliipa mechi uhai. Baadaye kidogo katika mitandao ya Kijamii msemaji wa timu, Haji Manara walau aliitia uhai.

Vinginevyo imepoteza uhai wake kwa sababu mashabiki wameumizwa na matokeo ya mechi zilizopita, hasa hii ya mwisho dhidi ya Al Ahly. Lakini pia wanataka kupeleka hisia zao kwa haraka katika mechi ya Yanga.

Kichwa changu kilikuwa na mjadala mmoja tu baada ya pambano la Alexandria. Simba ya Mohammed Dewji inataka nini ili ifikie anga za Al Ahly na AS Vita?. Kile kiwango cha Al Ahly kilinitisha sana. Lakini niliona fursa ya Simba kufikia anga za Al Ahly kwa mambo mawili.

Kwanza kabisa katika utajiri huu wa Dewji wanaweza kuanzisha ‘Shamba’ la wanasoka vijana kupitia viwanja vyao mbalimbali ambavyo wanaweza kutengeneza Bunju. Ndivyo ilivyo kwa Al Ahly. Wana vitalu vya vipaji. Lakini hapo hapo wana pesa za kununua mastaa wachache kwa bei mbaya. Hili la pili nadhani ni funzo pia. Kuwekeza kwa wachezaji wa bei mbaya zaidi. Walikuwa na wachezaji nane wa kigeni katika mechi dhidi ya Al Ahly lakini walipelekeshwa puta kama vile ni wachezaji wetu wa Temeke.

Al Ahly ina mchezaji wa Sh10 bilioni za Kitanzania. Kifupi wana mchezaji ambaye thamani yake inaziendesha Simba na Yanga kwa misimu miwili bila ya kuyumba. Wenzetu wameziweka katika mwili wa mchezaji mmoja tu. tutafika lini huku? Viko wapi vyanzo vya mapato? Tunawezaje kushindana na watu wa namna hii?

Akili za watu wa Simba sidhani kama zipo huku. Akili zetu zipo Februari 16. Simba imepania kumfunga Yanga mabao mengi kwa ajili ya kujipoza na kichapo cha mabao 5-0 mara mbili mfululizo. Simba ikishinda dhidi ya Yanga itasahau kila kitu. Unazisoma akili hizi kupitia mitandao ya kijamii.

Viongozi wa hizi timu hata kama wamekwenda Shule lakini wanaishi kwa presha za mashabiki. Nadhani hata ndani ya uwekezaji bado kuna mambo ambayo tunayaendesha kishabiki kwa kufuata hisia za mashabiki.

Siku tukijiwekea malengo makubwa na kusahau kidogo kuhusu upinzani wa jadi nadhani tutafika mbali. Haitakuwa mara ya kwanza Simba kumfunga Yanga mabao mengi lakini tumeishi hivi kwa muda mrefu bila ya kuona msaada unaotokana na matokeo ya aina hiyo. Tukirudi katika michuano ya kimataifa hali inakuwa vile vile.

Kiuchumi mechi ya Simba dhidi ya Al Ahly ina faida zaidi. Simba wakienda robo wanachuma mabilioni. Wakiifunga Yanga wanajiweka katika nafasi nzuri ya kuchukua ubingwa ambao mwisho wa msimu bingwa wake anazawadiwa Sh80 milioni.

Sijui tutaishi hivi mpaka lini. Tukiendelea kuishi hivi ina maana kwa miaka mingi ijayo tutaendelea kuwa wasindikizaji. Pindi timu moja inapokuwa na nguvu dhidi ya mtani wake basi inajiona imemaliza. Inamuwaza mtani badala ya kumfikiria mpinzani ambaye aliwapeleka puta katika mechi ya mwisho.

Matokeo ya Alexandria yamethibitisha nguvu kubwa ndani ya soka ya Tanzania bado haisaidii kukupa matokeo mazuri ya mechi za kimataifa. Inahitajika nguvu ya ziada kwa sababu tunacheza na wapinzani dhaifu. Bila kujali matokeo ya kesho wala yale ya wikiendi ijayo, Simba inabidi ijipime na kuonyesha njia ya kudumu kwa wengineo. Mfumo wao mpya wa uendeshwaji unapaswa kutuonyesha njia ambazo Al Ahly imefika na sio kufikiria matokeo ya Yanga au Azam.

Advertisement