Familia za soka Babu hadi Mjukuu

Muktasari:

Hakuna ubishi si kitu cha kawaida sana kushuhudia babu hadi mjukuu wote wakitamba kwenye soka, lakini hizi ni baadhi tu ya familia ambazo zimetamba kwenye soka la kiwango cha juu kizazi na kizazi kuanzia babu hadi wajukuu.

LONDON, ENGLAND. DUNIA imewahi kuwashuhudia wanasoka wa maana sana duniani na kitu cha kuvutia watoto wao na wajukuu zao wamefuata nyayo zao, huku wengine wakiwa maarufu zaidi kuliko vizazi vyao vilivyowatangulia kwenye mchezo huo.

Hakuna ubishi si kitu cha kawaida sana kushuhudia babu hadi mjukuu wote wakitamba kwenye soka, lakini hizi ni baadhi tu ya familia ambazo zimetamba kwenye soka la kiwango cha juu kizazi na kizazi kuanzia babu hadi wajukuu.

8. Maldini

Cesare Maldini alikuwa kizazi cha kwanza kwenye familia ya Maldini kutamba kwenye soka, tena kwenye klabu ya AC Milan akifanya hivyo kwa miaka 12. Maldini huyo babu alikuwa beki na alibeba mataji manne ya Serie A na Kombe la Ulaya mara moja. Kisha akaja, mtoto Paolo Maldini, kizazi cha pili huyo kwenye familia hii, naye alikuwa beki matata kabisa kuwahi kutokea duniani. Naye alicheza AC Milan kwa maisha yake yote, karibu miongo miwili, akishinda mataji saba ya ligi na matano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Na sasa imefika zamu ya mjukuu, Christian Maldini kuwakilisha familia hiyo, ambaye ndugu yake pia Daniel anafanya kweli. Kwa sasa anachezea kikosi cha AC Milan cha chini ya umri wa miaka 19, ambapo kwenye mechi za kujiandaa na msimu mpya, alichezea kikosi cha kwanza.

7. Marcos Alonso

Alonso ni ukoo mwingine uliotamba kwenye soka. Kizazi cha kwanza kwenye familia kutamba kwenye mchezo huo, alikuwa Marcos Alonso Imaz, aliyecheza kwenye timu nyingi tu ikiwamo Real Madrid, alikocheza kwa miaka minane. Alishinda La Liga mara tano na Kombe la Ulaya mara tano. Kizazi cha pili kilikuwa Marcos Alonso Pena, aliyekuwa winga na kuchezea wapinzani wa klabu ya baba yake, Atletico Madrid na Barcelona as well. Kwenye maisha yake ya soka alishinda La Liga mara moja na Copa Del Rey. Na kizazi cha sasa, kwa maana ya mjukuu, Marcos Alonso yeye ni beki wa kushoto, akikipiga kwenye kikosi cha Chelsea. Alonso mjukuu ameshinda Ligi Kuu England mara moja na Europa League.

6. Forlan

Juan Carlos Corazzo alikuwa wa kwanza kwenye kizazi cha Forlan kuwa mwanasoka, ambapo alizichezea timu kadhaa ikiwamo Indipendiente. Kwa bahati mbaya hakushinda taji lolote kwa klabu na timu yake ya taifa. Pablo Forlan alikuwa mkwe wa Corazzo, ambaye alikuwa akicheza beki. Pablo alishinda mataji ya ligi ya Uruguay mara saba na Copa Libertadores mara moja katika enzi zake za uchezaji.

Kisha akaja mjukuu, Diego Forlan ambaye amekuwa maarufu kuliko Forlan wengine wote waliomtangulia. Diego amecheza kwenye timu nyingi kubwa huko Ulaya kama Manchester United, Villarreal na Atletico Madrid, akishinda Ligi Kuu England mara moja na Europa League.

5. Gudjohnsen

Arnor Gudjohnsen kilikuwa kizazi cha kwanza kutoka familia hii ya wanasoka, ambapo alitamba kwenye timu kibao za huko kwao Iceland, Ubelgiji na Ufaransa. Alikuwa straika na ilibaki kidogo tu acheze na mwanaye, Eidur kwenye timu ya taifa kama si mtoto huyo asingepata majeruhi.

Baadaye, mtoto Eidur Gudjohnsen alikuja kuwa maarufu zaidi kwenye soka kuliko baba yake, akichezea Chelsea, Barcelona na Tottenham Hotspur.

Alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu England, La Liga moja na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kizazi hicho kimepita na sasa imekuja zamu ya wajukuu, ambapo watoto wawili wa Gudjohnsen wapo kwenye akademia ya Real Madrid, huku mtoto wake mkubwa, Sveinn Aron akitamba kwenye Serie B na kikosi cha Spezia Calcio.

4. Hernandez

Tomas Balcazar ni gwiji kwenye soka la Mexico, aliichezea Guadalajara na kushinda mataji manane katika kipindi cha miaka 10. Kisha akaja mkwe wake, Forlans, aliyekuja kutamba kwenye soka. Staa, Javier Hernandez Gutierrez maarufu kama Chicharo, aliyekuwa akicheza kiungo kwenye timu ya Tecos, Puebla FC na Monarcas Morelia, naye alitamba sana kwenye soka kutoka familia hiyo.

Baada ya hapo akaja mjukuu, Javier Hernandez Balcazar, aliyefahamika kama Chicharito, akitamba kwenye timu za Manchester United, Real Madrid na Bayer Leverkusen ni mwendelezo wa soka la kibabe kutoka kwenye familia hiyo. Chicharito alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu England na Klabu Bingwa Dunia mara moja.

3. Laudrup

Finn Laudrup wa kwanza kwenye familia hii kucheza soka, alipocheza kwenye timu kibao ikiwamo Brondby na Wiener Sportclub. Kwa bahati mbaya hakushinnda ubingwa wowote katika kipindi chake cha soka akiwa mchezaji. Kisha kikaja kizazi cha Michael Laudrup, ambaye alipata mafanikio kwenye soka akichezea Juventus, Barcelona na Real Madrid, huku akibeba mataji mengi tu, ikiwamo La Liga mara tano, Serie A moja na Kombe la Ulaya. ndugu yake, Brian Laudrup naye alikuwa mwanasoka na alikuwa akikipiga katika kikosi cha Bayern Munich na AC Milan, ambapo ameshinda Serie A mara moja na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Na sasa imefika zamu ya wajukuu, watoto wa Michael, Mads na Andreas ambao wote ni wanasoka japo si kwa kiwango cha juu, huku Brian naye mtoto wake Nicolai ni mwanasoka wakicheza timu moja na Mads ya mchangani Græsrødderne.

2. Koeman

Martin Koeman alikuwa kizazi cha kwanza cha soka katika familia hii na enzi zake alikuwa beki imara. Alichezea timu nyingi sana kama Groningen na Heerenveen. Aliichezea pia mechi moja timu ya taifa ya Uholanzi. Kisha kikaja kizazi cha Erwin na Ronald Koeman ambao pia walikuwa wanasoka, huku Ronald akibeba mataji ya kutosha tu katika vikosi vya Ajax, PSV Eindhoven na Barcelona. Alibeba mataji manne ya La Liga, manne ya Eredivisie na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Na sasa kuna mjukuu, Ronald Koeam Jr ambaye anachipukia akicheza kipa huko kwenye kikosi cha TOP Oss inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Uholanzi.

1. Kluivert

Kenneth Kluivert ni kizazi cha kwanza cha soka kwenye familia hii ya kina Kluivert, aliyekuwa akichezea Robinhood na Real Sranang na alichezea timu ya taifa pia. Wakati Patrick Kluivert akiwa maarufu zaidi katika familia hiyo, baada ya kucheza kwenye vikosi vya Ajax, AC Milan na Barcelona na kushinda mataji kibao, family hiyo iliendelea kutamba kwenye soka hadi wajuu. Mtoto wa Patrick, Justin Kluivert, ambaye ni mjukuu wa Kenneth Kluivert, kwa sasa ndiye anayetamba kwennye soka akikipiga kwenye kikosi cha AS Roma katika Serie A