Familia ya Samatta ni furaha tu, wachambuzi watoa neno

Monday July 27 2020
samattaa pic

STRAIKA wa Kimataifa, Mbwana Samatta amerejesha furaha katika familia yake, baada ya timu yake ya Aston Villa kubaki kwenye Ligi Kuu England, iliyomaliza nafasi ya 17 na pointi 35.

Wakati shangwe hilo likiendelea kwa Watanzania wengi, Baba mzazi wa staa huyo, Ally Pazi Samatta amefichua ukweli kwamba familia yake ilikosa raha kutokana na mwenendo wa Aston Villa na ilivyobaki waliliamsha shangwe na kushindwa hata kulala.

Mzee Samatta, amesema wakati anatazama mechi ya mwisho ya Aston Villa na West Ham iliyochezwa jana Jumapili, alikuwa na presha kwa kuwa ilibeba hukumu ya timu ya mwanae  kushuka au kubakia ligi kuu.

"Tumeitazama mechi hiyo kwa roho ngumu, kwani tulikuwa hatuna namna, nikaiambia familia yangu tumuombee Mbwana ili afanikiwe kubakiza timu ligi kuu na asionekane kama ameenda na mkosi," amesema.

"Baada ya kupata pointi moja ambayo imewabakiza ligi kuu, ilikuwa kama sherehe kwani hatukulala kwa furaha, tukimshukuru Mungu kusikia maombi yetu," amesema Mzee Samatta.

ALICHOONGEA NA MWANAE

Advertisement

Mzee Samatta amesema mwanae alimpigia simu, akielezea furaha yake yakubakiza timu kwamba ni jambo lililomuongezea thamani ya kazi yake akicheza msimu wa kwanza Ulaya.

Amesema aliwashukuru Watanzania kwa namna ambavyo walionyesha moyo wa kuishabikia timu hiyo, kwamba ilimpa moyo kujituma kwa bidii kuonesha anatambua mchango wao.

"Ameniambia Baba kitendo cha Watanzania kuifuatilia Aston Villa, kimenipa nguvu ya kujituma na kutamani kufanya makubwa ya kuipeperusha bendera ya Tanzania na kuwafungulia milango wengine," amesema.

Ameongeza kuwa "Sijawahi kumuona Mbwana akiongea kwa furaha kama siku ambayo ameibakiza timu nikagundua kwamba alikuwa hayupo sawa kutokana na furaha kumzidi," amesema.

KAKA MTU ATOA NENO

Kaka yake Mohamed Samatta ambaye anacheza KMC, naye hakusita kutoa la moyoni kwamba mdogo wake alikuwa anapambana na vitu viwili, kutokushuka daraja na kuendana na aina ya uchezaji wao.

"Amekuwa akiniambia mara kwa mara kuwa aina ya uchezaji wao, upo tofauti kabisa na timu ambazo amepitia, hivyo alikuwa anajifunza kuendana nao, huku akipambana isishuke," amesema.

"Ameelezea furaha yake kwamba timu hiyo kubakia ligi kuu, kutamfanya atimize ndoto zake za kufanya makubwa msimu ujao,"amesema Mohammed

Advertisement