Fabregas 'painia' wa EPL

Muktasari:

  • Wenger alimfanya Fabregas kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya Arsenal alipompa nafasi ya kucheza kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 16, kwenye mechi ya Kombe la Ligi dhidi ya Rotherham Oktoba 28, 2003.

TAKWIMU na makombe ni vitu vinavyoweza kukupa wazo juu ya athari aliyopata mchezaji wa zamani wa Arsenal na Chelsea, Cesc Fabregas kwa soka ya England.

Ameondoka kujiunga na Monaco wa Ufaransa atakakoungana na mchezaji mwenzake wa zamani wa Arsenal, Thierry Henry ambaye huko ni kocha, wakati Fabregas bado atakuwa anasukuma ndinga.

Fabregas aliwika sana Arsenal, baada ya kuwa amechukuliwa akiwa chipukizi kabisa kule Barcelona halafu baada ya kuwika vyema akiwa na Arsene Wenger alienda tena Barcelona; hakufanya vyema sana hivyo baada ya muda mfupi akaruhusiwa kuondoka, washabiki wa Arsenal wakadhani Wenger angemchukua lakini akampandishia ‘vioo’, huyoo akaenda Chelsea.

Leo Chelsea wanaye Kocha Maurizio Sarri, baada ya kuwa na kina Jose Mourinho na Antonio Conte na amekuwa na mipango tofauti hivyo hata wachezaji waliodhaniwa kuwa nyota na nguzo wanaonekana kutokuwa na nafasi hapo kama tulivyoona kwenye makala iliyopita.

Fabregas si tu unaweza kumwita ni mashine ya kuzalisha mabao kwa maana ya kutoa usaidizi kwa wafungaji, bali pia unaweza kwenda mbali zaidi na kusema huyu amekuwa ‘pioneer’ au kwa Kiswahili painia, akifanya upainia wa mabao uwanjani.

Kila nilipobahatika kumwona Fabregas, hata tangu akiwa tineja, nilimwona ni mchezaji wa aina ya Barcelona lakini angehimili mikiki ya Ligi Kuu ya England (EPL).

Aina ya uchezaji wake katika kiungo tumekuja kuiona nchini hapa England, ikiwa pia ni kutoka kwa watu kama David Silva na Bernardo Silva wa Manchester City, lakini ukweli ni kwamba alipowasili kutoka Akademia ya Barca, Fabregas alikuwa wa aina yake.

Kile wanachofanya kina Silva sasa – kucheza kwenye eneo kubwa zaidi la uwanja kwa muda mfupi na kufanya mambo makubwa kutokea ni kwamba Fabregas alikuwa akiyafanya miaka 15 iliyopita kwenye ule mfumo w a 4-4-2 kwa Arsenal... na kwa hakika aliwezesha mafanikio katika njia hiyo.

Hadi ‘alipotoboa’ na kuingia kwenye timu ya Arsenal 2003 akiwa na umri wa miaka 16 tu, timu ilipocheza dhidi ya Arsenal ni wachezaji walizoea kukutana na majitu.

Ghafla wakaja kukutana na kijana mdogo kwa umri na umbo katika Fabregas badala yake. Wangemwangalia na kujiuliza angeweza kuwafanya nini.

Wenger alimfanya Fabregas kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya Arsenal alipompa nafasi ya kucheza kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 16, kwenye mechi ya Kombe la Ligi dhidi ya Rotherham Oktoba 28, 2003. Alitwaa Kombe la FA miaka miwili tu baadaye na kucheza kwenye fainali ya Kombe la Mabingwa Ulaya (UCL) dhidi ya Barcelona 2006.

Japokuwa alikuwa mdogo, alikuwa amekomaa sana kwa umri wake, pia mwenye akili sana na anayeponyoka kiaina.

Alikuwa kiungo wa aina mpya na mgumu kwa wapinzani kukabiliana naye, hivyo kwamba baadhi ya wachezaji wanakiri hawakuwa wakitaka kupangwa kwenye eneo lake au kukutana naye kwa sababu alikuwa painia mzuri wa mabao na ngmu kumzuia.

Ni mchezaji mahiri si kwa maneno au kufikirika tu, pia kwa takwimu, kwa sababu zinaonesha kwamba anashika nafasi ya kwanza kwa EPL tangu katika kutengeneza nafasi, akiwa nazo 845 hadi anaondoka Chelsea wakati ameshika nafasi ya pili kwa kutoa usaidizi kwa mabao, akifanya hivyo mara 111 nyuma ya Ryan Giggs aliyefanya hivyo mara 162 na ameshastaafu.

Sasa hapo unaweza kuona Fabregas ni mchezaji wa aina gani, akifananishwa na hao kwenye takwimu na ieleweke hapo ni mmoja tu amebaki EPL – Silva, kwa hiyo ligi hii maarufu zaidi duniani imepoteza mwamba hasa. Pengine tumjumuishe na mstaafu mwingine katika Paul Scholes aliyekuwa ‘pass master’.

Kama washabiki wa Arsenal walivyosikitika kuondoka kwake na kocha kutotumia fursa iliyojitokeza kumsajili kwa mara ya pili, wale wa Chelsea pia watasikitika, japokuwa umri umekwenda sasa na ule ukali wake kupungua. Hata hivyo, bado alikuwa kifaa.

Akiwa tineja, ukweli, hakuwa mkali kwa pasi sana, maana alikuwa akikimbia zaidi na mpira lakini kadiri muda ulivyokwenda, umri kuongezeka, akaanza mambo ya pasi za uhakika, pengine moja ya sababu zikiwa kwa vile hakuweza kukimbia tena tofauti na awali.

Alikuwa mchezaji anayekimbia hapa na pale, hata arudi nyuma kwa golikipa wake kuchukua mpira, kisha anaondoka nao na kusogeza wenzake mbele, akiwaelekeza ya kufanya naye akiwa kama mwenye kuamuru mpira uende vipi. Muvu ikivurugika angerudi tena hadi kwa kipa na kutaka apewe mpira na ilikuwa ngumu mno kwa wapinzani wake kumshinda na kila mara alikuwa kwenye mpira au anakimbia. muda mwingi alikuwa timamu kimwili, timamu kuliko wengine wengi au kuliko hata ambavyo watu wengine wangefikiria.