Fabinho aumia azua balaa kwa Liverpool

Mercyside, England. Liverpool imeendelea kuingia katika matatizo ya safu ya ulinzi baada ya kiungo aliyerudishwa katika ukabaji, Fabinho kuumia katika mchezo wao wa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Midtjylland.

Kocha wa wekundu hao, Jurgen Klopp alimtaja beki huyo kama mtu muhimu aliyebaki katika safu yake ya ulinzi kwa ajili ya kuziba pengo lililoachwa na Virgil van Dijk.

Beki huyo wa kimataifa wa Brazil, alilazimika kucheza nafasi ya Van Dijk, lakini juzi usiku alicheza kwa dakika 60 kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Fabinho, ambaye sasa ana miaka 27, alionekana kuumia misuli ya paja na kulazimisha kutolewa uwanjani.

Mchezaji huyo wa Liverpool aliacha nafasi yake ikichukuliwa na kinda Rhys Williams na kuacha wasiwasi katika kikosi hicho cha Klopp.

Williams mwenye miaka 19, aliichezea Kidderminster Harriers katika mashindano ya Ligi ya Mataifa ya Ulaya msimu uliopita.

Jurgen Klopp sasa atakuwa na wakati mgumu wa kuchagua nani wa kuziba pengo la nyota huyo baada ya kupoteza nyota wa pili katika eneo la ulinzi.

Kocha huyo raia wa Ujerumani alisema: “Ilikuwa kama kitu cha mwisho kwetu. Sijui hata la kufanya kwakweli, alijisikia kama misuli yake ya paja haiko sawa.”