Fabinho abebeshwa lawama Liverpool

LIVERPOOL, ENGLAND. MKONGWE Graeme Souness amewataja mastaa watatu wa Liverpool, Fabinho, Naby Keita na Georginio Wijnaldum kuwa ndio waliohusika na kichapo cha mabao 7-2 kutoka kwa Aston Villa kwenye Ligi Kuu England Jumapili iliyopita.

Wachezaji hao watatu wote walianzishwa kwenye safu ya kiungo ya Liverpool kwenye mchezo huo, wakati staa mpya Thiago Alcantara alipokosekana kwa kuumwa corona na nahodha Jordan Henderson kuanzia kwenye benchi.

Kiwango cha hovyo kwenye mchezo huo kiliwafanya Liverpool kufungwa 4-1 hadi mapumziko kabla ya kukumbana na kipigo kikubwa zaidi kwenye ligi.

Baada ya mechi, kocha Jurgen Klopp hakutaka kumbebesha lawama yeyote yule licha ya kukiri kwamba timu yake ilipoteana na kufanya makosa mengi ambayo hayapaswi kufanywa kwenye soka.

Lakini, Souness anaamini viungo hao ndio wanaopaswa kubebeshwa lawama kutokana na kichapo hicho.

“Tatizo la Liverpool lilianzia na kuishia kwa watu hawa. Kiungo hiyo iliyoanzishwa, Fabinho, Wijnaldum na Keita,” alisema mkongwe huyo.

“Hawakufanya kazi yao ipasavyo. Kisha wakatoa na hata wale walioingia nao hawakufanya kazi yao inavyopaswa.”

Keita alitolewa na kuingia Takumi Minamino, lakini hat-trick ya Ollie Watkins iliwapa wakati mgumu zaidi Liverpool katika kutafuta matokeo mazuri katika mechi hizo.

Kisha Fabinho alirudishwa kwenye beki kuchukua nafasi ya Joe Gomez ili kumpisha James Milner kwenye kiungo na hakuna kilichofanyika.