Fabiano aeleza namna riadha ilivyompa utajiri

Muktasari:

  • Bingwa huyu wa zamani wa dunia wa mbio za nusu marathoni anasema, kama sio riadha, uenda leo hii asingekuwa maarufu, asingekuwa na kazi wala mijengo ya maana aliyojenga Arusha.

Dar es Salaam. Amepata kazi, amejenga nyumba tatu kali pale Arusha, kama haitoshi amewekeza katika miradi mbalimbali inayomuingizia kipato, huyu ni mwanariadha nyota wa timu ya Taifa, Fabiano Joseph.

Mwanariadha huyo hakusoma sana, lakini ametumia kipaji chake na kasi yake ya miguu kutengeneza kipato.

Bingwa huyu wa zamani wa dunia wa mbio za nusu marathoni anasema, kama sio riadha, uenda leo hii asingekuwa maarufu, asingekuwa na kazi wala mijengo ya maana aliyojenga Arusha.

“Nilizaliwa katika familia duni, kuna wakati nyumbani kwetu mvua ikinyesha, kama ni usiku, hakuna kulala tena, tunaamka kwani paa la nyumba lilikuwa likivuja, lakini kupitia riadha nimeboresha pia maisha ya familia yangu kijijini Gedamali,” anasimulia Fabiano.

Riadha

Fabiano anasema hakuna mchezo una pesa ya muda mfupi kama riadha sanjari na kumfanya mwanariadha kuwa nyota ndani ya kipindi kifupi sana.

Anasema mafanikio yake yalianza mwaka 2003 alipofuzu kushiriki mbio za dunia ambazo alichuana kwenye mita 5,000 na 10,000 na hakurudi nyuma baada ya kupata nafasi hiyo.

Mwaka huo pia Puma walimuona na kujitosa kumdhamini, anasema aliutendea haki mkataba wa Puma kwani mwaka uliofuatia alifuzu Olimpiki katika mbio za mita 10,000 ambazo aliingia fainali kwenye mtoano (heat).

Mbio zilizompa ulaji

Fabiano anasema alishinda mbio tofauti na kulipwa fedha nyingi, lakini mbio kubwa zilizompa fedha za nusu marathoni za dunia mwaka 2005 ambazo alikuwa bingwa kule Edmonton Canada.

“Nilishinda pia medali ya pili kwenye mbio za Dubai marathoni ambako nililipwa Dola 100,000, hii ilikuwa fedha kubwa kuipata kwenye riadha, Puma waliniongezea bonasi pia.

“Muda wa saa moja ulibadili maisha yangu, kwa mafanikio haya na fedha hii ambayo kama ningekuwa msomi nisingeweza kulipwa mshahara kama huo ndani ya saa moja katika muda wa kazi ila kwenye riadha inawezekana.

Mali

Ukiachana na kibarua alichopata Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) mwaka jana, Fabiano Joseph amejinasua kwenye umasikini kupitia riadha huyo.

Nyota huyo pale Arusha ana miliki mijengo mitatu ya maana, mmoja ukiwa wa ghorofa ambako ndiko anaishi eneo la Ilboru.

“Nyumba nyingine ipo visiwani upande wa Sanawali ambako nimepangisha Wazungu na nyingine ina vyumba 24 iko kwa Mrombo ambayo iko mbioni kukamilika na nitaifanyia biashara pia.

Mbali na nyumba hizo, Fabiano ambaye ana mpango wa kustaafu timu ya Taifa mwakani kwenye Olimpiki ya 2020 kule Japan ana gari ya mchanga ambayo inamuingizia kipato kila wiki Sh 800,000.