FKF imefulia? Kocha wa Stars hajalipwa miezi mitatu

Muktasari:

  • Kocha wa timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars, Mfaransa Sebastien Migne, ameipatia shirikisho la soka nchini (FKF), makataa ya siku 10 (hadi Oktoba 15), kulipa mishahara yake ya miezi mitatu (Julai, Agosti na Septemba), la sivyo atachukua hatua.

Nairobi, Kenya. Unaweza kuhisi ni utani au hekaya za abunuasi, lakini ukweli ni kwamba ya kufanya kazi kubwa tangu achukue mikoba ya kuinoa timu ya taifa, Harambee Stars, Mfaransa Sebastien Migne hajalipwa mishahara ya miezi mitatu.

Unaposikia hili unaweza ukahisi ni uzushi wa mitaani. Hata hivyo kwa mujibu wa kauli ya Rais wa shirikisho la soka nchini (FKF), Nick Mwendwa ni kweli kwamba Migne hajalipwa mshahara wa mwezi Julai, Agosti na Septemba na sasa ametishia kumwaga mboga!

Ndio, akizungumza mapema leo, Mwendwa alisema FKF, kwa sasa inapitia wakati mgumu huku akikiri kuwa Migne amelipatia shirikisho hilo makataa ya siku 10 (hadi Oktoba 15) kumlipa fedha anazodai la sivyo atachukua hatua ambayo haitawafurahisha wengi.

 “Ni kweli kwamba hajalipwa kwa kipindi cha miezi mitatu. Ametuambia tumalize deni hilo kabla ya Oktoba 15, la sivyo atachukua hatua, lakini hajaweka wazi ni hatua ipi. Tunapambana kuhakikisha tunamlipa mshahara wake,” alisema Mwendwa.

Kucheleweshwa kwa mshahara wa Mfaransa huyo kunadaiwa kuathiri mipango yake kwa timu ya taifa iliyoingia kambini jana huku ikitarajiwa kuondoka kesho kuelekea Ethiopia kwa ajili ya mechi ya kufuzu 2019 AFCON, itakayopigwa Oktoba 10.

 “Unajua baadhi ya hawa makocha hawajazoea mazingira yetu haya ya utendaji kazi, makubaliano yakishafikiwa ni ngumu kubadilishwa. Ukikubaliana nao kuhusu jambo fulani hasa swala la malipo lazima utimize,” aliongeza Mwendwa.