FKF: Kiingilio bure mechi Starlets, Ghana

Muktasari:

Kenya imepangwa Kundi B, pamoja na mabingwa watetezi Nigeria, Zambia na Afrika Kusini. Mechi yao ya kwanza itapigwa Novemba 18, dhidi ya Shipolopolo ya Zambia. Kwa Upande wao wenyeji Black Queens ya Ghana, wapo kundi A, sambamba na Algeria, Mali na Cameroon.

Nairobi, Kenya. Mashabiki wa soka Kenya watashudia bure kirafiki kati ya timu ya taifa ya Kenya ya Wanawake, Harambee Starlets dhidi ya wenzao Black Queens ya Ghana utakaochezwa kwenye Uwanja wa Moi Kasarani, Jumatano ya Novemba 7.

Naam habari ndio hiyo, kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirikisho la Soka nchini (FKF), kwenda kwa umma wa wapenda michezo nchini, iliyowekwa kwenye mtandao wa shikrikisho hilo, ni kwamba wananchi wameombwa kujitokeza kuishangilia Starlets, kwani hakutakuwa na kiingilio Uwanjani Kasarani.

“Tunapenda kutoa rai kwa Wakenya kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu yetu. Dada zetu wanatuhitaji zaidi. Tujitokeze kujaza uwanja wa Kasarani na kuwaongezea morali. Kama shirikisho tutahakikisha kila mtu anapata nafasi ya kuishangilia Starlets, na hivyo hakutakuwa na kiingilio,” ilisomeka taarifa ya FKF.

Agizo la kufuta kiingilio katika mtanange huo wa kujipima ubavu, ni sehemu ya juhudi ya FKF, chini ya uongozi wa Nick Mwendwa kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kutoa sapoti kwa timu hiyo inayojiandaa na michuano ya kombe la mataifa ya Afrika, itakayotimua vumbi kuanzia Novemba 17 hadi Desemba mosi, mwaka huu, nchini Ghana.

Baada ya kuvaana na Ghana, vijana wa Kocha David Ouma, watawaalika majirani zao Uganda katika mchezo mwingine wa kirafiki ambao ni wa mwisho kabla ya kukwea pipa, Novemba 14, kuelekea Accra Ghana, kwa ajili ya AWCON, ambayo pia itatumika kama mechi za kufuzu fainali za kombe la Dunia kwa wanawake, itakayofanyika mwakani.