Wameanza Hat Trick za kwanza ligi kuu za ulaya

Mambo yameanza kunoga mapema sana. Ulaya inanoga licha ya janga la corona. Kwenye ligi kubwa huko kuanzia ya Ujerumani, Hispania, Italia, Ufaransa na ile maarufu ya England, mambo ni moto na mashabiki kwa sasa wako bize kweli kufuatilia mambo yanavyokwenda.

Achana na mabao mengi huku ligi zikiwa mbichi tu lakini kuna mastaa wameanza na kasi ya kutupia mabao matatumatatu yaani hat trick.

Kwenye Ligi Kuu England (EPL) na ile ya Ujerumani (Bundesliga) na Ligue 1 ya Ufaransa, usipime kabisa na hawa ndio mastaa walioingia kambani mara tatu na kusepa na mipira yao.

MEMPHIS DEPAY-lyon

Utamu wa ligi za Ulaya ulianmzia hapa na ni kama aliwakumbusha wengine nyavu zinatikiswa tu.

Ndiye aliyefungua ubao wa namba tatu ‘hat trick’ kwa timu za ligi tano bora Ulaya baada ya ligi ya Ufaransa Ligue 1 kutangulia kuanza huku akiisaidia Lyon kushinda mabao 4-1 dhidi ya Dijon.

Mohammed Salah - Liverpool

Liverpool ikiikaribisha Leeds United iliyopanda daraja, katika mchezo ambao wengi wanaamini ndio mechi ya kibabe zaidi kushuhudiwa kwenye raundi hii ya kwanza ya msimu, vijana wa Jurgen Klopp, walijikuta wakitumia nguvu nyingi, kupata ushindi wa 4-3, kazi kubwa ikifanywa na ‘mfalme wa Misri’, Mohamed Salah.

Mabao matatu ya mguu wa kushoto ya ufundi mkubwa, yalimshuhudia Salah, akijiweka kwenye rekodi kama mchezaji wa kwanza kupiga hat trick ya kwanza, katika msimu wa 2020/21 kwenye EPL.

Salah alifunga mabao katika dakika ya 4, 33 na 88, mawili akifunga kwa mkwaju wa penalti. Bao la nne la Liverpool liliwekwa kimiani na Virjil van Dijk (dk 20) huku mabao matatu ya Leeds yakifungwa na Jack Harrison, Patrick Bamford na Mateusz Klich (12, 30, 66).

Calvert Lewin - Everton

Ndio habari ya mjini pale Goodison Park baada ya kujiweka kwenye rekodi ya msimu huu wa EPL, kwa kuwa mchezaji wa pili, kupiga hat-trick. Zilimchukua dakika 31, 62 na 66 kufanya hivyo, katika ushindi wa 5-2 walizopata dhidi ya ya West Brom kwenye mchezo wao wa Jumamosi.

Serge Gnabry - Bayern Munich

Kampeni ya msimu wa 2020/21 wa ligi kuu ya Ujerumani, ulianza rasmi Septemba 18. Kulikuwa na mchezo mmoja tu, uliowahusisha mabingwa wa Ulaya, Bayern Munich, wanaotetea taji lao la Bundesliga. Schalke 04 walikutana na balaa pale Allianz Arena.

Bavarian waliendeleza dozi ya mabao 8-0, waliyoitoa msimu uliopita dhidi ya Barcelona. Schalke 04, huku karamu hii ikiongozwa na nyota wa zamani wa Arsenal, Serge Gnabry. Mfaransa huyo, aliyekuwa sehemu mafanikio ya kikosi cha Kocha Hans-Dieter “Hansi” Flick, kilichotwaa mataji matatu msimu uliopita, alifunga hat trick ya kwanza ya Bundesliga dakika ya 4, 47 na 59. Mabao mengine yalifungwa na Lewandowski, Leroy Sane, Leon Goretzka, Thomas Mueller na Jamal Musiela.

Heung-Min Son - Tottenham Hotspurs

Alikuwa na siku nzuri kwenye mchezo wa Jumapili dhidi ya Southampton baada ya kupasia kambani mara tatu ‘hat trick na kuondoka na mpira wake. Son aliiongoza Spurs, kuondoka na ushindi wa 5-2 ugenini, akitupia kambani mara nne, dakika ya 45, 47, 64 na 73. Bao la tano lilifungwa na Harry Kane, huku ya Southampton, yakiwekwa na Danny Ings.