Eymael apangua kikosi Yanga ikiwavaa wachovu Singida United

Muktasari:

Yanga imefanya mabadiliko nane katika kikosi chake cha kwanza kitakachoshuka Uwanja wa Taifa saa chache zijazo kuwakaribisha Singida United.

Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael amefanya mabadiliko nane katika kikosi chake kitakachoshuka uwanja wa Taifa kukutana na Singida United katika mechi ya Ligi Kuu Bara.

Eymael katika ukuta wake wa leo amemrudisha beki Lamine Moro pekee ambaye alicheza mchezo wa Simba na kupoteza kwa mabao 4-1 ambaye atacheza sambamba Kelvin Yondani huku kulia akianza Paul Godfrey 'Boxer' wakati kushoto akiwa Adeyun Saleh.

Safu ya kiungo nayo imekumbana na mabadiliko ambapo Abdulaziz Makame, Deuse Kaseke na Raphael Daud wakipewa nafasi ya kuanza.

Safu ya ushambuliaji mshambuliaji David Molinga ameendelea kuaminika na Eymael akianza sambamba na Mrisho Ngassa na Patrick Sibomana.

Eymael amelazimika kuwakosa wachezaji wake wawili beki Said Juma na kiungo Feisal Salum ambao wanatumikia adhabu ya kukosa mchezo mmoja kwa kufikisha kadi tatu za njano.

Pia hali ya kutokuwa sawa kwa kiungo Haruna Niyonzima na nahodha wao Papy Tshishimbi pia kumelazimisha mabadiliko hayo ambapo hata katika mazoezi ya timu hiyo wamekuwa wakikosekana tangu kupita kwa mchezo dhidi ya Simba.

Kwenye wachezaji wa akiba Eymael amewaweka kipa Ramadhan Kabwili, mabeki wakiwa Ally Mtoni,Japhar Mohamed wakati washambuliaji wakiwa Ditram Nchimbi, Yikpe Garmien,Eric Kabamba na kinda Adam Kiondo.