Eymael aonya : Mtusamehe hatuwaachi Singida

Tuesday January 21 2020

Eymael aonya - Mtusamehe hatuwaachi Singida -Yanga -Singida United-Luc Eymael -Mwinyi Zahera-

 

By Waandishi wetu

WAKATI Yanga ikitua mjini Singida kuikabili Singida United kesho, kocha mkuu wa timu hiyo, Luc Eymael amesema anauchukulia mchezo huo kama fainali ya ubingwa ili kupata matokeo kutokana na kuanza vibaya tangu alipokabidhiwa timu hiyo.

“Kwa kocha mkubwa kama mimi kuanza vibaya mechi mbili mfululizo sio jambo zuri kabisa na linaniweka katika wakati mgumu, hivyo tumejipanga kupambana kwa kila hali ili kupata matokeo mazuri dhidi ya Singida United,” alisema kocha huyo alipozungumza na Mwanaspoti jana.

“Nimeanza kuwafuatilia wapinzani wetu wanavyocheza kupitia CD za michezo yao ya nyuma, nafahamu wanavyoshambulia na kukaba, ingawa uwanja (wa Leti) sio rafiki kama ulivyo wa Taifa lakini bado hatutatoka mchezoni, tutatafuta ushindi.

“Mechi hii inanipa picha juu ya kazi yangu ndani ya Yanga, hivyo ni lazima nipambane kupata ushindi maana naona kikosi changu kimeimarika kwa kiasi kikubwa.”

Eymael amejaza nafasi ya Mwinyi Zahera na katika mechi mbili alizokiongoza kikosi hicho, Mbelgiji amepoteza zote; ya kwanza ikipokea kipigo cha maba0 3-0 kutoka kwa Kagera Sugar na 1-0 dhidi ya Azam mechi ambazo zilichezwa jijini Dar es Salaam.

Alisema anakwenda Singida kwa lengo moja tu ambalo ni kupata ushindi ingawa anatambua kuwa mchezo wa soka una matokeo matatu; kufungwa, sare na kupoteza huku akisisitiza kwamba hataki kusikia habari ya hayo mengine mawili kwani ushindi ndio umeshikilia hatima ya kibarua chake.

Advertisement

Mbali ya dhamira aliyonayo, Mbelgiji huyo pia aliweka wazi matatizo yanayoikabili timu yake uwanjani akisema safu ya ushambuliaji kushindwa kuona lango na tatizo la mawinga ndiyo mambo yaliyompa wakati mgumu katika mechi hizo mbili alizosimamia.

“Mapungufu hayo nimeyafanyia kazi, hata ukiangalia mechi yetu na Azam tulijitahidi ingawa safu ya ushambuliaji haikuwa na makali kwenye umaliziaji. Mawinga pia wana mapungufu, naamini mechi ijayo tutakuwa na matokeo mazuri kwani ndiyo lengo pekee kwetu.

Singida nao kukaza

Wakati Eymael akijinasibu kumalizia hasira za kufungwa kwa Singida United, kocha mkuu wa timu hiyo, Ramadhan Nsanzurwimo amesema hawatishwi na ukubwa wa jina la Yanga na wataelekeza nguvu zao kuvuna pointi tatu ili kujinasua kwenye nafasi ya pili kutoka mkiani katika msimamo wa ligi hiyo.

Alisema wanaichukulia Yanga kama timu nyingine za Ligi Kuu, na kwamba wachezaji wake wapo vizuri kisaikolojia, wakiwa na morali ya juu ya kupambana katika mchezo huo.

“Tunashukuru kwanza kucheza kwenye uwanja wetu wa nyumbani, hakuna sababu ya kupoteza alama tatu tukiwa hapa kwa sababu tuna wachezaji wanaoweza kupambana kupata matokeo mazuri,” alisema.

Yanga shingo upande

Yanga iliondoka jana kwenda Singida ikiwa na manung’uniko ya kubadilishiwa ratiba kwani awali, mechi hiyo ilipangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha kesho kabla ya kuhamishiwa kwenye Uwanja wa Leti, Singida.

Katibu Mkuu wa Yanga, Dk David Ruhago alisema hatua hiyo ya kubadilishiwa uwanja imeitia hasara timu yao kwani ilikuwa imefanya malipo ya awali kwenye hoteli moja jijini humo ikiwamo tiketi za ndege.

“Hatujafurahishwa kubadilishiwa ratiba, tuliandikiwa barua ya kucheza Arusha lakini ghafla imebadilika, tunawaomba viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi tunapoandika barua zijibiwe,” alisema.

Imeandikwa na Thobias Sebastian, Thomas Ng’itu na Gasper Andrew

Advertisement