Evergreen wazipigia hesabu pointi za Marsh

Muktasari:

  • Nyango alisema waliwatazama Marsh Queens walipocheza dhidi ya Yanga Princess na kudai wamebaini mbinu zao hivyo hawatapata tabu kutimiza malengo yao.

BAADA ya Evergreen kuanza kwa kichapo cha mabao 12 wakifungwa na JKT Queens mabao 5-0 na Simba Queens mabao 7-0 sasa wanajipanga kumalizia hasira kwa Marsh Queens, watakayocheza nayo Ijumaa ya wiki hii.

Kocha wa Evergreen, Omary Nyango alisema wamejipanga kuhakikisha wanaonja ushindi raundi ya pili dhidi ya Marsh Queens ambao ni wageni wao.

Nyango alisema waliwatazama Marsh Queens walipocheza dhidi ya Yanga Princess na kudai wamebaini mbinu zao hivyo hawatapata tabu kutimiza malengo yao.

“Tutacheza na Marsh ambao wametuzidi pointi mbili na hata kwenye msimamo wao wapo nafasi ya tisa sisi ya 10 itakuwa mechi ngumu lakini tumedhamiria ushindi.

“Raundi ya pili kila timu inataka ushindi nyumbani utakaomtengenezea mazingira ya kujiweka nafasi salama, kikosi changu kipo sawa na wachezaji wana kiu ya kuonja ushindi,” alisema.

Alisema kuwa kwa sasa wanachokifanya ni kuhakikisha wanapambana kufanya vizuri katika mechi zilizo mbele yao na kuwa na matokeo mazuri kwa siku za mbele.