Evander sasa kung'ata sikio la Mike Tyson!

NANI alitarajia kwamba Mike Tyson atamng’ata sikio mpinzani wake Evander Holyfield kwenye pambano lao la pili lililofanyika mwaka 1997 tena mara mbili? Kila utakayemuuliza atakwambia hakutarajia. Na ndivyo ilivyo hata kwa Evander mwenyewe ambaye amebaki kutoamini hadi leo kwamba aling’atwa na Tyson.

Baada ya Evander kufanikiwa kumtandika Tyson kwenye pambano lao la kwanza mwaka 1996 na mwaka mmoja uliofuata kurudiana, kila mmoja alitarajia Tyson alipize kisasi.

Lakini Tyson alishangaza wengi kwa kushindwa kumaliza pambano hilo kwa kosa la kumng’ata mara mbili Evander akitoa sehemu ya juu ya sikio lake na kumpa ushindi wa ‘bwerere’ ukiwa ni wa pili dhidi yake ndani ya mwaka mmoja.

Nini kitatokea? Bila ya shaka umeshasikia kuhusu pambano namba tatu baina ya Tyson na Holyfield ambalo linatajwa kufanyika wakati huu wote wawili wakiwa na umri ambao ni mgumu kuchapana makonde kama ilivyowahi kuwa wakati wa miaka hiyo walipopigana mara mbili.

Upo uwezekano mkubwa wa maveterani hao kupigana pambano maalum la hisani kuchangisha fedha ambapo wote wawili wamethibitisha kuwa wako tayari kupigana na hapo ndipo ambapo Evander amefichua kwamba alikaribia kidogo kulipiza kwa kumng’ata Tyson alipomng’ata mara ya kwanza akajizuia na ndipo hakutarajia Tyson kumng’ata tena mara ya pili.

Evander alisema kabla ya kulipiza akawa amepewa ushindi kwa makosa hayo ya Tyson.

Ushanifahamu? Itakuwaje ikitokea wakapigana kwenye pambano hilo la hisani pindi ikitokea Mike Tyson akamzidi vitasa, Evander. Jamaa hataamua kumng’ata Tyson ikawa kama kulipiza kisasi cha kuwahi kung’atwa wakati ule?