Etienne:Nawafatilia wapinzani wangu

KOCHA mkuu wa timu ya Taifa Tanzania 'Taifa Stars', Etienne Ndayiragije ameweka wazi kwamba anawafahamu wapinzani wake ambao atakutana nao katika hatua ya kufuzu Kombe la Mataifa Afrika na Kombe la Dunia.

 "Nawafatilia Tunisia kwa ukaribu na najua kwamba tarehe 13 wanacheza mchezo wa kirafiki na Nigeria, najua kabisa wakiwa nyumbani wanakuwa bora zaidi, pia timu hii ina wachezaji wengi wanaocheza Ligi ya kwao, wanatoka mara moja kwenda nje ya nchi yao lakini wanarudi tena kwao" amesema Ndayiragije.

 Akizungumzia upande wa wachezaji ambao amewaita lakini wadau wamekuwa wakihoji sana amesema yeye anaamini kabisa kwamba watafanya kitu  kikubwa katika kikosi chake.

 "Mfano niliwahi kumuita Nchimbi walihoji lakini ni mchezaji mwenye nguvu, mbio na anajua kuficha mpira, hii pia ni mechi ya kirafiki nimeita hawa, pia kuna wachezaji kama watano walinipigia simu wakaniuliza kwanini sijawaita nikawaambia wanifanyie kazi kwa sababu bado kuna CHAN" amesema.

AFICHUA MAOVU YA KLABU ZA LIGI KUU

Etienne alisema wakati wa mazoezi amekuwa akitembelea viwanja mbalimbali vya mazoezi ambapo timu za Ligi Kuu huwa wanafanya mazoezi, ameona Simba ndio timu pekee ambayo inakuwa inataka magoli kwni imekuwa ikiwafundisha  wachezaji  wake kufunga.

"Timu nyingi yani zinakuwa zinecheza mchezo wa kupasiana (Open Space) na wanahesabiana mpaka 10 na inakuwa pointi moja, hii sio nzuri kwa sababu kwenye mechi kinachohitajika ni magoli, hata jana niliongea na Lyanga (Ayoub) wa Azam nilimpa mfano hai kwamba Prince Dube anagusa mpira mara moja na kwenda golini, hata Mugalu na yeye anafanya hivyo lakini yeye anakimbia pembeni na kwenda kwenye kona ili apige krosi, nilimuambia abadilike kidogo".

Kocha huyo amefunguka zaidi na kusema hata upande wa makipa pia kumekuwa na changamoto kubwa kwa wachezaji hao kutotumika kama sehemu ya kikosi kwani wanapewa mazoezi ya peke yao.

Ndayiragije amesema suala la makipa wa Tanzania imetokana na madhara ya namna ambayo yanatokana na klabu za Ligi Kuu, kwani wanapewa mazoezi ya peke yao na zinapobaki dakika 15 wakiwa wamechoka ndio wanaitwa.

"Wakati wachezaji wanapewa mazoezi na makipa nao wanatakiwa wawepo ili wajue sehemu ambayo wanasimama, wakati unafundisha jinsi ya kucheza kipa anatakiwa awepo, mazoezi ya makipa kama makipa inatakiwa mapema labda asubuhi ndio wafanye lakini kwa jioni lazima waungane na wenzao".

"Nchi nyingi makipa ndio makapteni kwa sababu wanakaa kwa muda mrefu kwenye timu, kuna muda watu waliuliza kwanini nimemuita Kaseja, lakini mimi nilimfundisha kuwa kama nahodha halafu kama kocha kwa sababu yeye anapokuwa nyuma ndio anaona timu nzima,", amesema Ndayiragije

AFUNGUKIA ISHU YA FARID MUSSA

Winga Farid Mussa aliyesajiliwa na Yanga akitokea katika kikosi cha CD Tenerife inayocheza Ligi Daraja la Pili nchini Hispania safari hii hajajumuishwa katika kikosi cha Stars huku kocha Ndayiragije akisema bado mchezaji huyo ana nafasi lakini anatakiwa kupambana.

"Farid ni mchezaji mzuri na namfatilia vizuri nina imani atakuja kuwa na msaada  baadae, kwa sasa anatakiwa kwanza atulie tu katika klabu yake (Yanga) na pambane ili kunusuru kipaji chake" amesema Ndayiragije. Winga huyu katika mechi nne za Ligi Kuu alikuwa hapati nafasi ya kucheza katika kikosi cha Yanga hali ambayo iliibua maswali mengi kutoka kwa wapenzi na wadau mbalimbali wa soka nchini.

 Kikosi cha Stars tayari kiko  kambinikujiandaa na mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi itakayopigwa Oktoba 11 katika uwanja wa Benjamin Mkapa.

 Himid Mao atawasili Jumatano akitokea Misri, Simon Msuva na Nickson Kibage wataingia siku hiyo usiku kutoka Morocco  wakati huo huo Ally Msengi yeye tayari ameshaingia nchini akitokea Afrika Kusini.