Eti Ole anafukuzwa kazi

Friday July 12 2019

 

LIVERPOOL, ENGLAND.STAA wa zamani wa Liverpool na Aston Villa, Dean Saunders amesema Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer hatoboi na atafutwa kazi msimu huu kama hatafanya usajili wa wachezaji wake mwenyewe.
Saunders alisema Ole yatamkumba yaliyowakumba wenzake huko Old Trafford kwamba kuna hatari asimalize msimu akafukuzwa kama ataendelea kubaki na kundi kubwa la wachezaji waliopo kwenye kikosi cha sasa na kushindwa kufanya usajili wa wachezaji wake mwenyewe ambao watapambana kwa ajili yake.
Solskjaer, 46, ataanza msimu wake wa kwanza mzima mzima kwenye kikosi hicho cha Old Trafford, lakini tayari hadi sasa mambo yanaonekana yatakwenda kuwa magumu kwa upande wake msimu ujao.
Msimu uliopita timu ilimaliza ligi kwenye nafasi ya sita huku ikiachwa nyuma kwa pointi 32 na vinara Manchester City. Hadi sasa wachezaji ambao Solskjaer amewasajili katika kikosi hicho ni makinda winga, Daniel James na beki wa kulia Aaron Wan-Bissaka.
Alipoulizwa kama anadhani Solskjaer atabaki kuwa kocha wa Man United hadi msimu ujao, Saunders, 55, alisema: “Sidhani kama atakuwepo. Naona alivyoingia kwenye matatizo na kazi ngumu inayomkabili. Wachezaji hawa waliopo sasa Man United ni wachezaji ambao wamehusika wakati makocha watatu walipofutwa kazi. Wachezaji hawahawa wamemfanya Mourinho afutwe kazi, hivyo kama Solskjaer hatasajili wachezaji wake, atafukuzwa pia, ipo hivyo.”
Komenti za watu huko kwenye mitandao ya kijamii wanadai Solskjaer akifika Krismasi ya mwaka huu na hajafutwa kazi basi ni mwanamume.

Advertisement