Eti Mourinho hafiki Krismasi

Wednesday September 16 2020

 

LONDON,ENGLAND. BALAA hilo. Kocha Jose Mourinho ana nafasi nne kati ya tano za kufutwa kazi Tottenham Hotspur kabla ya Krismasi, mwaka huu baada ya kuchapwa na Everton kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu England.

Spurs iliduwazwa kwa kichapo nyumbani na chama la kocha Carlo Ancelotti Jumapili iliyopita, wakati Everton iliposhinda 1-0. Kwenye mchezo huo, Spurs ilionekana dhaifu ndani ya uwanja huku Everton ikitawala muda wote, ikipata huduma bora kutoka kwa wachezaji wapya James Rodriguez, Allan na Abdoulaye Doucoure.

Na wacheza kamari wanadai Mourinho kwenye nafasi tano za kufutwa kazi - kuna nne za uwezekano wa Mreno huyo kuonyeshwa mpango wa kutokea na bosi Daniel Levy kabla ya kufika Krismasi.

“Hakuna namna ambayo Jose ataendelea kuwa kocha wa Spurs hadi kufika mwisho wa msimu kama matokeo hayatabadilika. Kwa kifupi, tunadhani atafukuzwa kabla ya Krismasi,” ilifichua taarifa ya wacheza kamari hao.

Kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, Spurs imefanya usajili wa wachezaji wawili tu - kiungo wa Southampton, Pierre-Emile Hojbjerg na beki wa kulia wa Wolves, Matt Doherty. Taarifa zaidi zinafichua Mourinho yupo kwenye mchakato wa kumnasa Alexander Sorloth, ambaye alifunga mabao 32 kwenye klabu ya Trabzonspor alikocheza kwa mkopo msimu uliopita. Baada ya kipigo cha Jumapili, Mourinho aliwashutumu wachezaji wake akidai ni wavivu.

Advertisement