Eti Bale kama vipi ahame tu Madrid

Tuesday May 14 2019

 

MADRID, HISPANIA.GARETH Bale atafute tu timu ya kwenda kuichezea maana maisha yameshakuwa magumu huko Real Madrid. Staa huyo hata kwenye kikosi hakuwekwa wakati Zinedine Zidane alipotaja timu yake iliyokipiga na Real Sociedad juzi Jumapili.

Hata hivyo, hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Bale kupigwa chini kwenye kikosi cha Zidane, ikitokea kwa wiki ya pili mfululizo wakienda kuchapwa na Sociedad 3-1.

Kocha Zidane kwa vitendo vyake hivyo ameonyesha wazi Bale hana maisha katika kikosi hicho cha Bernabeu huku wakala wake, Jonathan Barnett akitunisha misuli akisema mchezaji wake haendi kokote.

Mkataba wa Bale bado una miaka mitatu kwenye timu hiyo ambayo inamlipa Pauni 500,000 kwa wiki, lakini mabosi sasa wanahangaika kutafuta timu ya kumsukumia huko.

Zidane alisema mchezaji huyo ni mzima, lakini hakutaka tu kumjumuisha kwenye kikosi chake na hivyo kuamua kumpa nafasi Brahim Diaz.

Zidane alisema: “Sijui kama atacheza dhidi ya Real Betis. Tuone itakavyokuwa wiki ijayo. Wikiendi hii yameshafanyika yamekwisha.”

Advertisement

Diaz aliifungia Real Madrid bao la kuongoza, lakini Mikel Merino, Joseba Zaldua na Ander Barrenetxea waliifungia Sociedad na kumlaza mapema kocha Zidane kwa kipigo kizito.

Advertisement