Esperance yaipiga Al Ahly nje ndani yatwaa ubingwa Afrika

Muktasari:

Esperance iliyofungwa mabao 3-1 katika fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika jana usiku ilifanikiwa kuandika historia baada ya kupindua matokeo kwa kuifunga kwa mabao 3-0 Al Ahly ya Misri katika mechi ya pili ya fainali hivyo kutwaa taji kwa jumla ya mabao 4-3.

Tunis, Tunisia. Hatimaye Esperance ya Tunisia imefanikiwa kupindua matokeo baada ya jana usiku kuichapa Al Ahly ya Misri kwa mabao 3-0 katika mechi ya pili ya fainali na hivyo kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 4-3.

Katika mchezo wa kwanza wa michuano hiyo, Al Ahly ikiwa nyumbani Alexandria iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 hivyo ilihitaji sare ya aina yoyote kuweza kutwaa ubingwa nane wa Ligi hiyo.

Shujaa wa mchezo huo wa jana kwa wenyeji alikuwa ni mchezaji wa akiba, kiungo Saad Bguir 24, aliyefunga mabao mawili yaliyosaidia ushindi huo wa tatu kwa klabu hiyo.

Bguir alipatya nafasi ya kuanza katika mchezo huo, kutokana na Franck Kom kutumikia adhabu ya kadi iliyomgharimu kukosa mchezo.

Baada ya mchezo huo kocha wa Esperance, Moïne Chaâbani alisema kuwa ushindi huo ni uthibitisho kuwa malalamiko yao yalikuwa ya kweli kwamba Al Ahly ilibebwa katika fainali ya kwanza ndiyo maana ikashinda kwa 3-1, ambapo ilipewa penalti mbili za utata.

Alitamba kuwa licha ya mchezaji wao mmoja kulimwa kadi nyekundu hapo jana wakiwa kwenye dimba lao la Olympique de Rades walithibitiosha ubora wao.

“Tumethibitisha kuwa Al Ahly ilibebwa katika fainali ya kwanza ilipewa penalti mbili kwa msaada wa teknolojia ya bao VAR,” alisema.

Esperance, iliyotwaa ubingwa mwaka 1994 na 2011, italiwakilisha bara la Afrika katika michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia itakayochezwa Desemba mwaka huu katika nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu.