England yafanyiwa vitendo vya ubaguzi Bulgaria

Muktasari:

England imejikuta katika mazingira magumu katika mchezo wake dhidi ya Bulgaria, baada ya wachezaji kufanyiwa vitendo vya ubaguzi.

Sofia, Bulgaria. Licha ya kubaguliwa, England imepata ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Bulgaria katika mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Ulaya.

England ilicheza katika mazingira magumu baada ya mashabiki wa Bulgaria kuwafanyia vitendo vya ubaguzi wachezaji wenye asili ya Afrika.

Raheem Sterling aliyefunga mabao mawili aliandamwa sana na mashabiki hao waliokuwa wakimuita nyani. Mabao mengine yalifungwa na Marcus Rashford, Ross Barkley (mawili) na Harry Kane.

Mchezo ulilazimika kusimama mara mbili baada ya wachezaji wa England kumvaa mwamuzi wakipinga vitendo vya mashabiki hao.

Kocha wa England Gareth Southgate aliwatuliza wachezaji wake na mara kadhaa alikwenda kulalamika kwa mwamuzi kuhusu matukio hayo.

Mchezo huo ulisimama dakika ya 43 baada ya Southgate kutoa malalamiko kwa mwamuzi kabla ya kuendelea. Awali ulisimama dakika ya 28.

“Niliona kundi la watu wapatao 50 wakiwa wamevaa mavazi ya rangi nyeusi wakitoa ishara mbaya ikiwemo saluti yenye mrengo na masuala ya kiasa,”alisema Mwenyekiti wa Chama cha Soka Greg Clarke.

Ufaransa ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Uturuki, Kosovo iliilaza Montenegro mabao 2-0, Lithunia ilicharazwa 2-1 ilipovaana na Serbia, Iceland ilichapwa 2-0 dhidi ya Andora na Albania ilishinda 4-0 ilipomenyana na Moldova.