Emmanuel Okwi aunguruma Simba

Saturday March 16 2019

 

By Doris Maliyaga

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi raia wa
Uganda, amewaambia mashabiki wanataka kuvuka pamoja hatua ya robo fainali, hivyo lazima wawepo kwa wingi Uwanja wa Taifa leo Jumamosi kwa sababu ni siku yao.


Okwi ambaye alikosa mchezo uliopita na JS Saoura ya Algeria kwa
sababu ya maumivu lakini upo uwezekano mkubwa kuwa sehemu ya mchezo kulingana na mipango ya Kocha Patrick Aussems katika mechi hiyo na AS Vita ya Congo inayotarajiwa kupigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


Amesema: "Katika mchezo huu na AS Vita tunawahitaji sana
mashabiki wetu ili tupambane pamoja. Tunataka kufanya siku ya
leo tuwe pamoja kwa sababu mmekuwa mkituunga mkono kila mechi hadi tukafika hapa lengo ni kuvuka pamoja hatua inayofuata ya robo fainali."


Simba na AS Vita inacheza mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi kwa Kundi D, pamoja na Al Ahly ya Misri na JS Saoura ya Algeria.


Timu zote nne, zinacheza leo wakati Simba anakipiga na AS Vita,
Al Ahly wao watakuwa wanacheza na JS Saoura nchini Misri.


JS Saoura ndiyo vinara wa Kundi D, wanaongoza kwa pointi nane,
Al Ahly ni ya pili ina pointi saba ambazo ni sawa na za AS Vita
wakitofautiana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa, Simba wao wanashika mkia na pointi sita.


Timu zote zina nafasi ya kusonga mbele hatua ya robo fainali
kama zitafanya vizuri kwenye michezo yao hiyo ya mwisho.

Advertisement