Emery kijasho chamtoka kuhusu mabeki Arsenal

Muktasari:

  • Kwenye mechi ya juzi, Koscielny alikuwa benchi, lakini hakuwa fiti kiasi cha kumfanya Kocha Emery asimchezeshe baada ya Mustafi kuumia kwenye kipindi cha pili.

LONDON, ENGLAND.ARSENAL imekumbwa na majanga ya kupoteza mabeki wake wengi kwa majeruhi baada ya Shkodran Mustafi naye kuumia kwenye mechi ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Huddersfield kwenye Ligi Kuu England.

Beki huyo Mjerumani alilazimika kutoka uwanjani baada ya kupata maumivu ya misuli na nafasi yake ilichukuliwa na Nacho Monreal, ambaye ndiyo kwanza naye alikuwa akirudi uwanjani kutokea kwenye majeruhi.

Beki mwingine wa Arsenal, Rob Holding ameumia na hatacheza tena msimu huu. Kuna beki Sokratis Papastathopoulos, ambaye atakosa mechi ijayo ya ligi dhidi ya Southampton baada ya kuonyeshwa kadi ya tano ya njano msimu huu katika mechi ya juzi Jumamosi.

Kutokana na hilo, Kocha Unai Emery sasa anakuwa kwenye wakati mgumu wa kuwakosa mabeki wake wa kati muhimu kabisa katika mwezi huu wenye mechi kibao za kucheza. Monreal alirudi kucheza mechi ya kwanza tangu Oktoba baada na kusumbuliwa na maumivu ya misuli, wakati Laurent Koscielny bado hajawa fiti na anachokifanya kwa sasa ni kujifua tu mazoezini baada ya kuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha miezi saba.

Kwenye mechi ya juzi, Koscielny alikuwa benchi, lakini hakuwa fiti kiasi cha kumfanya Kocha Emery asimchezeshe baada ya Mustafi kuumia kwenye kipindi cha pili.

Arsenal ina mechi sita za kucheza kabla ya kufika Januari ambapo dirisha dogo la usajili litakuwa wazi kusajili kama kutakuwa na ulazima huo wa kufanya hivyo.