Emery awakaba koo Man United

Muktasari:

Kocha Emery ameifanya Arsenal kuwa na makali zaidi ya Man United kwenye Ligi Kuu England na kutamba ndani ya Top Four msimu huu wakati kikosi cha Jose Mourinho kikiwa nafasi ya nane

UNAI Emery ndio kiboko ya Manchester United. Amewafanya mashabiki wa wababe hao wa Old Trafford kufunga midomo yao, huku akiwafanya wale wa Arsenal kutamba kwa sababu hawacheki tena na timu za kitoto.
Kwenye Ligi Kuu England, Arsenal na Man United zote zimecheza mechi nane, lakini chama la Emery lina poingi 18, mbili tu nyuma ya vinara Manchester City waliofungana pointi na Chelsea na Liverpool.
Pointi hizo 18 zinawafanya Arsenal kushika nafasi ya nne. Hao Man United na kocha wao Jose Mourinho, kwenye mechi nane walizocheza, wamekusanya pointi 13 tu, wapo kwenye nafasi ya nane huko. Hilo tu linawafanya mashabiki wa Man United kuwa kimya, wasiizungumzie tena Arsenal.
Wakati upande mmoja ukiwa kimya, huko kwa wababe wa Emirates mashabiki wao wanaulizwa maswali, kwani wao na Man United wanacheza lini. Kwenye Ligi Kuu England, msimu huu, Arsenal imeshinda mechi sita, wakati Man United imeshinda mbili tu. Kitu kingine ambacho Emery ameipoteza Man United ni kwamba Arsenal yake imechapa timu zote zinazoonekana kuwa ndogo kwenye ligi hiyo, lakini Man United vichapo vitatu ilivyopokea vyote kutoka kwa timu ndogo.
Bado haijacheza na wale wababe kama Liverpool, Man City na Chelsea. Mechi ijayo itaanza na kibarua cha kuikabili Chelsea ya Eden Hazard.
Huko nyuma, Arsenal ilikuwa ikichapwa na vigogo na kuchapwa na timu vibonde pia. Lakini msimu huu chini ya Emery, inapiga tu. Arsenal imezichapa Fulham, Everton, Cardiff City, Newcastle United, Watford na West Ham United.
Imepigwa na vigogo tu, Man City na Chelsea, tena hizo zilikuwa mechi mbili za mwanzo za msimu. Man United imechapwa na West Ham na Brighton, lakini ikitoka sare na Wolves, huku mechi nyingine iliyopigwa ni ile ya Tottenham Hotspur.
Man United imechapwa hadi ya Derby County, timu ndogo, ambayo kwa Arsenal ya msimu huu inapiga tu bila ya shida.
Kwa kasi hiyo, mastaa wa Arsenal kama Alexandre Lacazette, Pierre-Emerick Aubameyang, Mesut Ozil na Matteo Guendouzi wanawaumbua masupastaa wa Man United wanaolipwa pesa ndefu kama Paul Pogba, Romelu Lukaku, Alexis Sanchez na hata staa mpya Fred, kwamba wao si kitu kama wanashindwa kupata matokeo kwa timu ndogo, vipi watakapowakabili vigogo wengine wa Big Six, wakiwamo Arsenal wenyewe.
Hivyo ndivyo Arsenal ilivyowafunga midomo Man United msimu huu!


SUMMARY
Kocha Emery ameifanya Arsenal kuwa na makali zaidi ya Man United kwenye Ligi Kuu England na kutamba ndani ya Top Four msimu huu wakati kikosi cha Jose Mourinho kikiwa nafasi ya nane