Emery amtaka Pepe atue Arsenal

Thursday October 11 2018

London, England. Kocha wa Arsenal, Unai Emery anajiandaa kutuma ofa kwa ajili ya winga wa klabu ya Lille ya Ufaransa, Nicholas Pepe anayewaniwa pia na Bayern Munich ya Ujerumani.
Emery amesema nia yake ni kujenga kikosi imara cha ushindani na anaamini winga huyo atakuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi chake kinachopambana kurejea kwenye nne bora ‘top four’ za Ligi Kuu England.
“Kikosi chetu kimeanza kuimarika, lakini bado tunahitaji kuimarisha baadhi ya maeneo nadhani tunahitaji winga mwenye kasi ili kusaidia upatikanaji wa mabao,” alisema Emery bila kufafanua.
Pepe ameshafunga mabao sita katika Ligi Kuu Ufaransa ‘Ligue 1’ msimu huu anaonekana atakuwa chache ya mabao kwa washambuliahji wapya wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette.
Washambuliaji hao waliosajiliwa na kocha Arsene Wenger hawakuwa na mafanikio ndani ya klabu hiyo katika mechi za mwisho za msimu uliopita, lakini wamekuwa moto msimu huu chini ya Emery.
Kocha huyo aliyeanza msimu huu vibaya akipoteza mechi mbili za kwanza kwa kufungwa an Manchester City na Chelsea, baada ya hapo ameshinda mechi zote sita zilizofuata kiasi kwamba hivi sasa ameanza kuonekana kuwa tishio hata katika mbio za ubingwa.
Kikosi cha Emery kwa sasa kipo pointi mbili tu nyuma ya City, Chelsea na Liverpool zilizo kileleni, lakini kiwango kilichoonyeshwa na vijana wake kimewastusha wachambuzi wengi na kusema anaweza kuzipiku timu hizo kabla ya Krismas.
Kocha huyo pia ameweka bayana hatakubali kumuuza mchezaji yeyote katika dirisha la usajili la Januari kama hakuna ulazima wa kufanya hivyo.

Advertisement