Emery afungua milango kwa Mustafi, Elneny Arsenal

Muktasari:

Kiungo, Elneny, 27, ambaye alianzishwa kwenye mechi tano tu za ligi msimu uliopita, ameshindwa hata kuwekwa benchi kwenye mechi mbili walizocheza msimu huu. Dirisha la usajili huko Ulaya linafungwa Septemba 2 na Emery amewashauri wachezaji hao waende wakajaribu bahati zao kwingineko.

LONDON, ENGLAND. KOCHA wa Arsenal, Unai Emery amewaambia Shkodran Mustafi na Mohamed Elneny waondoke kwenye kikosi chake haraka kabla ya dirisha la usajili huko Ulaya halijafungwa.
Emery amewaweka wazi wachezaji hao wote wawili kwamba watasugua sana benchi kama wataendelea kung'ang'ania kwenye kikosi hicho hadi dirisha la usajili huko Ulaya litakapofungwa.
Mustafi, 27, amekuwa akikosolewa sana na mashabiki kuhusu kiwango chake cha msimu uliopita, ambapo makosa aliyofanya ndani ya uwanja yaliigharimu sana timu hiyo. Na sasa ujio wa David Luiz na kupanda kiwango kwa Calum Chambers kunamfanya Mustafi awe na nafasi finyu ya kupata nafasi licha ya kwamba msimu uliopita alicheza mechi 31 kwenye Ligi Kuu England.
Kiungo, Elneny, 27, ambaye alianzishwa kwenye mechi tano tu za ligi msimu uliopita, ameshindwa hata kuwekwa benchi kwenye mechi mbili walizocheza msimu huu. Dirisha la usajili huko Ulaya linafungwa Septemba 2 na Emery amewashauri wachezaji hao waende wakajaribu bahati zao kwingineko.
Alisema: "Ni wachezaji wakubwa sana, lakini kutokana na mambo yalivyo, wakibaki hata watapata nafasi chache sana za kucheza, dakika chache sana. Ninachowatakia ni heri. Nadhani kitu bora kwao ni kwenda kwenye timu nyingine kukumbana na changamoto mpya.”
Mustafi amekuwa akihusishwa na mpango wa kutimkia huko kwenye Serie A kujiunga na AS Roma kwa dili la Pauni 23 milioni, huku Bordeaux wao wakionyesha dhamira ya kumsajili Elneny, lakini kila kitu kwa sasa kimesimama.