MAFUNDI : Eden Hazard anavyoongoza timu mabao huko England

Muktasari:

  • Hii ndio orodha ya wachezai waliohusika kwa mabao mengi kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

LONDON, ENGLAND.HUKO kwenye Ligi Kuu England utamu umekolea. Liverpool wanashika usukani wa ligi hiyo, huku mastaa Mohamed Salah na Pierre-Emerick Aubameyang wakichuana vikali katika kufukuzia Kiatu cha Dhahabu.

Hapo kwenye suala la kufunga kuna wachezaji wamehusika kwenye mabao mengi sana msimu huu kwa maana yale waliyofunga na waliyoasisti kwa wenzao wafunge kuzisaidia timu zao kwenye kusaka ushindi.

Hii ndio orodha ya wachezai waliohusika kwa mabao mengi kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

6. Sergio Aguero- mabao 12 Amefunga 8, asisti 4

Kinara wa mabao wa muda wote huko Manchester City, Sergio Aguero alikuwa pengo kubwa wikiendi iliyopita wakati timu hiyo ilipomenyana na Chelsea kwenye Ligi Kuu England.

Man City walianza mechi hiyo bila ya huduma ya mshambuliaji wao huyo na hakika hilo limewafanya kukosa mengi.

Hata hivyo, Aguero bado amekuwa mchezaji muhimu kwa kuhusika kwenye mabao mengi kwenye Ligi Kuu England msimu huu, akihusika kwenye mabao 12 baada ya kufunga manane na kuasisti mengine manne.

Aguero ndiye silaha hatari ya kocha Pep Guardiola huko Man City kwenye kufunga mabao.

5.Callum Wilson- mabao 13 Amefunga 8, asisti 5

Straika wa Bournemouth, Callum Wilson amekuwa akifurahia msimu wake bora kabisa kwenye huko Ligi Kuu England.

Mwingereza huyo amehusika kwenye mabao 13, akifunga mara nane na kuasisti mengine matano.

Wilson ni mmoja wa washambuliaji ambao wamekuwa wakiwapa mastaa wengine kama Mohamed Salah changamoto katika kutikisa nyavu.

Kitu ambacho kitawafanya wachezaji kama Wilson kushindwa na akina Aubameyang ni kutokana na timu zao ndogo wanazochezea, inakuwa ngumu kukwepa vipigo wanapokutana na vigogo.

4.Pierre-Emerick Aubameyang- mabao 13 Amefunga 10, asisti 3

Mshambuliaji wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang amezidi kumdhalilisha fowadi wa Manchester United, Alexis Sanchez kutokana na makali yake anayoonyesha kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Staa huyo wa kimataifa wa Gabon amehusika kwenye mabao 13 msimu huu, akifunga mara 10 na kuasisti mabao matatu.

Huko kwa Sanchez mambo ni magumu na kutokuwa na maajabu yoyote kwenye kikosi cha Man United baada ya kujiunga nacho akitokea Arsenal kwenye dirisha la Januari mwaka huu kipindi ambacho Aubameyang naye alitua Arsenal akitokea Borussia Dortmund.

3.Raheem Sterling- mabao 14 Amefunga 8, asisti 6

Mshambuliaji wa Manchester City, Raheem Sterling amegonga vichwa vya habari wiki hii kwa sababu zisizokuwa za mpira.

Fowadi huyo Mwingereza alilalamika kufanyiwa ubaguzi na mashabiki wa Chelsea katika mechi ambayo Manchester City walichapwa 2-0 uwanjani Stamford Bridge.

Amevishutumu vyombo vya habari pia kwa kulichochea jambo hilo na kufanya suala la ubaguzi liendelee kuwapo kwenye mchezo wa soka.

Achana na hilo, kwenye Ligi Kuu England mchango wa Sterling huko Man City ni mkubwa akihusika kwenye mabao 14, ambapo amefunga manane na kuasisti mengine sita.

2.Mohamed Salah- mabao 14 Amefunga 10, asisti 4

Fowadi wa Liverpool, Mohamed Salah alifunga hat-trick dhidi ya Bournemouth na hivyo kupanda juu kabisa katika msimamo wa vinara wa mabao kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Lakini, kama utaunganisha mabao yake aliyofunga pamoja na asisti alizotoa, basi Mo Salah anazidiwa na mtu mmoja tu, Eden Hazard tena kwa kuhusika kwenye bao moja zaidi.

Mo Salah amehusika kwenye mabao 14, akifunga 10 na kuasisti mengine mane na hivyo kuifanya Liverpool kuwa na kitu cha kujivunia kwenye ligi hiyo kwa msimu huu.

1.Eden Hazard- mabao 15 Amefunga 7, asisti 8

Kocha wa Chelsea, Maurizio Sarri lazima atakuwa anapasua kichwa kwa sasa kutafuta sababu za kumfanya staa wake Eden Hazard apunguze kasi yake ya kufunga.

Mbelgiji huyo alianza msimu kwa kasi sana na kufunga mabao saba kwenye Ligi Kuu England, lakini kwa miezi ya karibuni amekuwa mvivu kwenye kufunga na kinachoongezeka labda ni asisti tu.

Hata hivyo, bado anakuwa mchezaji aliyehusika kwenye mabao mengi zaidi kwenye Ligi Kuu England msimu huu akihusika kwenye mabao 15, akifunga saba na kuasisti manane.