Ed presha Old Trafford haimtishi ,anapiga pesa

Muktasari:

MANCHESTER United wapo nafasi ya 12 kwenye msimamo. Kocha, Ole Gunnar Solskjaer yupo kwenye wakati mgumu, lakini mtu aliyekuwa kwenye wakati mgumu zaidi ni Ed Woodward.

MANCHESTER, ENGLAND.  MANCHESTER United wapo nafasi ya 12 kwenye msimamo. Kocha, Ole Gunnar Solskjaer yupo kwenye wakati mgumu, lakini mtu aliyekuwa kwenye wakati mgumu zaidi ni Ed Woodward.

Baada ya kusemwa sana makocha kuanzia kwa David Moyes, Louis van Gaal, Jose Mourinho na sasa Solskjaer kwa kuonekana hawafai, ghafla sasa kibao kimegeuka na kuonekana Ed Woodward kuwa ndiye tatizo.

Ed Woodward ndiye bosi kubwa huko Man United. Akihusika kwenye dili zote za usajili. Analalamikiwa kuwa shida kwa sababu amekuwa hasajili wachezaji wanaotakiwa na makocha kwa wakati.

Mfano tu kwenye dirisha lililopita amewauza wachezaji wenye uzoefu kama Romelu Lukaku, Alexis Sanchez, Marouane Fellaini na Ander Herrera na kubaki na wachezaji wasiokuwa na uzoefu, huku akiwasajili Harry Maguire na makinda Aaron Wan-Bissaka na Daniel James. Ndiyo sasa ipo hovyo, imechapwa mara tatu kwenye mechi nane za Ligi Kuu England ilizocheza hadi sasa na kuachwa pointi 15 na vinara Liverpool.

Na sasa kumekuwa na madai kutoka kwa watu kwamba Ed Woodward afutwe kazi. Je, jambo hilo linaweza kumtetemesha?

Ripoti zinadai kwamba Ed Woodward ni moja ya mameneja wanaolipwa pesa nzuri jambo linalomfanya kuwa na kipato kinachokadiriwa kuwa Pauni 10 milioni.

Akifahamika kwa majina yake halisi, Edward Gareth Woodward, alizaliwa Novemba 9, 1971 huko Chelmsford, Essex. Alisoma katika shule huko Brentwood na kusomea Fizikia kwenye Chuo Kikuu cha Bristol, lakini baadaye alikwenda kusomea uhasibu na kuhitimu mwaka 1996. Tangu hapo akaanza kunasa dili za kupiga pesa ndefu kama vile kwenda kufanya kazi Man United.

Mkwanja wa Ed

Bosi huyo anaripotiwa kuwa na pato la Pauni 10 milioni.

Kazi yake nzuri anayofanya huko Man United kwenye wigo wa kibiashara, umemfanya Ed awe analipwa mshahara mkubwa pamoja na bonasi kibao.

Mambo ya timu ndani ya uwanja si mazuri, lakini Ed amejitahidi kuhakikisha Man United inanasa dili nyingi za kibiashara na kujikuta akiingizia timu pesa za kutosha na kupata bonasi nyingi tu. Ripoti zinadai kwamba mshahara wake kwa mwaka Ed ni Pauni 2.521 milioni, pesa ambayo ni kubwa kuliko meneja mwingine yeyote anayelipwa kwenye Ligi Kuu England. Kitu hicho ndicho kinachomfanya bosi huyo kuwa na pesa za kutosha na kumiliki mkwanja huo mrefu kwenye akaunti zake za benki, Euro 10 milioni. Ukichanganya na bonasi kwa mwaka Ed anachukua hadi Pauni 4 milioni.

Makazi na familia

Kuwa bosi wa klabu kubwa kama Man United, bila ya shaka makazi ya Ed hayawezi kuwa ya kawaida kawaida. Bosi huyo anaishi kwa raha sana licha ya kuwa na presha kubwa ya kuingoza Man United ya mashabiki wengi karibu kila kona ya dunia hii. Bosi huyo anaishi na mkewe kipenzi, mrembo Nicole Capuano, ambaye walifunga ndoa mwaka 1989. Hakuna ubishi, Ed anaishi maisha yake kwa raha sana.