Dylan Kerr aifuata Everton

Muktasari:

Gor Mahia ilipata fursa ya kuwa timu ya kwanza kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kwenda nchini Uingereza kucheza mechi ya kuwania kombe dhidi ya klabu yenye hadhi kubwa kama Everton, baada  ya kutetea ubingwa wao wa kombe la Sportpesa kwa kuifunga Simba SC ya Tanzania 2-0, ugani Afraha, Nakuru, mapema mwaka huu.

Nairobi, Kenya. Kuelekea mechi ya kirafiki kati ya mabingwa mara mbili wa kombe la Sportpesa, Gor Mahia dhidi ya Everton FC ya Uingereza, Kocha wa Gor Mahia, Muingereza Dylan Kerr, anatarajiwa kuhudhuria mechi ya Everton dhidi ya Crystal Palace, kuiba uchawi wao.
Ikiwa ni moja ya mbinu ya kujiandaa na mchezo huo, Kerr amepanga kuwasoma Everton wakiumana na Crystal Palace huku pia akitarajia kutumia muda wake mapumziko akiwa nchini Uingereza kushuhudia mechi kati ya Hull City na Preston, kabla ya kurejea nchini kukisuka kikosi chake.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoifikia Mwanaspoti Digital ni kwamba, Muingereza ambaye amefanikiwa kuipatia Kogalo ubingwa wa ligi kuu mara mbili, Kombe la Sportpesa Super Cup mara mbili, Super Cup moja pamoja na kufuzu klabu bingwa Afrika mara mbili, aliondoka nchini leo kuelekea Uingereza kwa ajili ya mapumziko.
Mbali na mechi hiyo ya Everton, Gor Mahia ambao ni mabingwa watetezi wa KPL, wataanza kampeni ya kutafuta taji la la 18, watakaposhuka dimbani Desemba 8, mwaka kuumana na Bandari FC, ugani Mbaraki, mjini Mombasa, kwa mujibu wa ratiba ya msimu mpya wa 2018/19, iliyotolewa jana.
Pia Kogalo watacheza mechi ya kufungua pazia la msimu mpya dhidi ya mshindi wa Kombe la FKF Shield Cup, utakaozikutanisha klabu ya Karobangi Sharks na Sofapaka. Mechi hiyo ya ufunguzi wa ligi, itachezwa Desemba 2, mwaka huu.