Durant majanga, Raptors yaloa kwa Warriors

Tuesday June 11 2019

 

By Matereka Jalilu

Dodoma. Toronto Raptors wakicheza nyumbani Scoatiabank Arena wameshindwa kumaliza kazi waliyoifanya ugenini (Oracle Arena) uwanja wa Golden State Warriors wiki iliyopita waliposhinda mechi zote mbili mfululizo.

Ushindi huo ulikamilisha mechi nne za awali kwa Raptors kuongoza kwa matokeo ya 3-1 na walikuwa wanatakiwa kushinda mchezo mmoja uliofuata leo Jumanne.

Mchezo huo ulimalizika kwa Toronto Raptors kufungwa na Golden State Warriors pointi 105-106 wakishindwa kumalizia mchezo katika dakika moja ya mwisho na kuwaruhusu Warriors kushinda kwa pointi moja pekee.

Kyle Lowry wa Raptors alikosa nafasi mbili ambazo kama angefunga mojawapo ukiwemo mtupo wake wa pointi tatu aliorusha kutokea katika kona uliogonga juu ya nyuma ya ubao ambao kama ungeingia ungeipa ushindi na kubeba taji hilo wakiwa nyumbani.

Nyota Kawhi Leonard alifunga pointi 12 katika robo ya nne akimaliza na pointi 26 na Ribaundi 12 wakati Kyle Lowry alifunga pointi 18,Marc Gasol 17,Serge Ibaka 15,Pascal Siakam 12 na Fred VanVleet 11.

Ushindi wa Golden State Warriors kwa kiasi kikubwa ulichangiwa Stephen Curry na Klay Thompson kupitia pointi 3 zao walizofunga katika dakika tatu za mwishoni ambazo ndizo zimeipa ushindi dhidi ya Raptors.

Advertisement

Curry alifunga pointi 31, ribaundi nane na asisti saba, Klay alimaliza na pointi 26 wakati Draymond Green aliongoza kwa Ribaundi 10 na asisti nane.

Durant aumia tena

Baada ya Golden State Warriors kufungwa kwenye mechi zote mbili wakiwa uwanjani kwao Oracle Arena, jina la Kevin Durant lilitajwa zaidi kuwa ndiye atakayeiokoa Warriors na kufanya maajabu katika mechi ya leo Scoatiabank Arena.

Durant alifanikiwa kuanza katika mchezo wa leo akitoka katika majeraha yake ya mguu yaliyomuweka nje kwa muda mrefu tangu alipoumia kwenye mchezo wa tano wa nusu fainali ya ukanda wa  Magharibi dhidi Houston Rockets mwezi uliopita na kukosa mechi zote tisa zilizopita.

Hata hivyo nyota huyo hakumaliza kipindi cha kwanza, aliumia baada ya dakika tatu za robo ya pili ya mchezo huo akitonesha mguu wake wa kulia na kuugulia maumivu yaliyomfanya kuwa nje kwa muda mrefu.

Wakati anatoka alikuwa ameshafunga pointi 11 na ribaundi mbili ambapo nyota mwenzake Steph Curry alikiri kupata hali tofauti ya kupambana baada ya kuguswa na uamuzi wa Durant kujitosa kupambania timu yake kabla ya kuumia tena.

Mchezo ujao wa sita wa fainali hiyo utachezwa Alfajiri ya Ijumaa katika uwanja wa Oracle uliopo Oakland California nyumbani kwa Golden State Warriors.

Warriors watalazimika kushinda tena mchezo huo ili kuipeleka fainali ya mechi saba itayochezwa usiku wa Jumatatu ijayo.

Advertisement