Dullah Mbabe avuliwa ubingwa wa dunia

Muktasari:

Akiwa bingwa wa dunia wa WBO, Mbabe alichezea kipigo ndani ya siku 75 baada ya ubingwa huo kwenye pambano lisilokuwa la ubingwa dhidi ya Rocky Fielding.

BONDIA nguli wa zamani, Emmanuel Mlundwa ametaja sababu za bondia Abdallah Pazi (Dullah Mbabe) kuvuliwa ubingwa wa dunia wa WBO.
Hivi karibuni, WBO ilitangaza kumvua bondia huyo namba moja nchini kwenye uzani wa super middle mkanda huo alioutwaa Agosti mwaka jana kule China.

Mtanzania huyo alimchapa kwa Technical Knock Out (TKO) Zulipikaer Maimaitiali aliyekuwa akicheza nyumbani kwenye ukumbi wa TSSG Center, Qingdao na kutwaa ubingwa wa World Boxing Organisation Asia Pacific.
Akiwa na taji hilo kwa miezi minne, WBO ilitangaza kumvua na kutomtambua Mbabe kama bingwa wake wa dunia kwenye uzani wa super middle.
Tukio hilo limemuibua Mlundwa, ambaye ametaja sababu mbili zilizopeleka Mbabe kuvuliwa taji hilo.
"Alipaswa kulitetea ndani ya miezi mitatu lakini hakutokea promota wa kumuandalia pambano, lakini alipokwenda Uingereza kupigana pambano lisilo la ubingwa angewataarifa WBO," alisema.

Alisema akiwa Uingereza Mbabe alipigwa kwa Knock Out (KO na Rocky Fielding ), jambo ambalo anaamini limechangia WBO kuamua kumvua ubingwa wao.