Dullah Mbabe: Nipigwe na Twaha Kiduku!

Muktasari:

Alidai hapa nchini hajaona bondia wa kumsumbua, japo alikuwa akimuogopa Thomas Mashali (Marehemu) ambaye huyo kama angekuwepo ndiye angeweza kumpiga lakini sio Twaha.

BONDIA Abdallah Pazi (Dullah Mbabe) amewasikia baadhi ya wadau wa ngumi wakimzungumzia kuwa si mbabe tena, wadau hao hawakuishia hapo wamemtaja Twaha Kassim (Kiduku) kuwa ndiye kiboko ya Dullah.

Kama haitoshi wamemtabiria Dullah Mbabe kipigo cha Knock Out (KO) kama atakubali kupigana na Twaha Kiduku huku wengine wakisisitiza pambano hilo hata Dullah Mbabe aweke hela ya maana hawezi kulikubali.

Sasa buana jamaa kaamua kuvunja ukimya kwa wadau hao akisisitiza kuwa kati ya mabondia ambao hajawahi kuwahofia ni Twaha Kiduku pamoja na kwamba ndiye bondia namba moja kwenye uzani wa middle na Dullah Mbabe ni namba mbili.

“Mimi nimhofiea Twaha Kiduku! tena ikitokea amenipiga basi huo ndiyo utakuwa mwisho wangu ulingoni, yule bado bwana mdogo sana kwangu,” alitamba Dullah Mbabe ambaye mara ya mwisho alimpiga Francis Cheka kwa KO, Desemba mwaka jana.

Alisema hamhofii Twaha Kiduku na yuko tayari kucheza naye hata Leo kama ikitokea promota wa kuandaa pambano hilo.

“Najua uwezo wangu uko vipi katika ngumi, nimewasikia watu wanaodhani kuwa namuogopa Twaha Kiduku, hizo ni fikra zao siwezi kuzizuia, lakini Twaha anipige! haiwezi kutokea,” alisema.

Alidai hapa nchini hajaona bondia wa kumsumbua, japo alikuwa akimuogopa Thomas Mashali (Marehemu) ambaye huyo kama angekuwepo ndiye angeweza kumpiga lakini sio Twaha.

“Nilikuwa namuogopa Mashali, alikuwa anajua ngumi, anatembea ulingoni ana mbinu nyingi, mbishi, hachoki, lakini sio Twaha ameingia kwenye ngumi karibuni na anacheza mapambano mepesi tu,” alijiansibu Dullah Mbabe.

Twaha Kiduku ana rekodi ya kucheza mapambano 19, ameshinda mara 14 (7 KO), amepigwa mara na sare moja tangu 2013 alipoingia kwenye ngumi za kulipwa.

Wakati Dullah Mbabe ana rekodi ya kucheza mapambano 32, ameshinda mara 25 (22 kwa KO), amepigwa mara 6 na sare moja tangu 2013.