Dulla Mbabe, Kiduku lazima mtu apasuke

Thursday July 30 2020

 

By Mwandishi wetu

MABONDIA wenye upinzani mkubwa wa jadi Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ na Twaha Kiduku watamaliza ubishi wao Agosti 28 katika pambano la ubingwa wa Uhuru la uzani wa Super middleweight.

Hili ni pambano la pili kwa mabondia ambapo  Oktoba 21 mwaka 2017 walitoka sare katika ukumbi wa Msasani Club, sare ambayo ililamaikiwa na mashabiki wa ngumi za kulipwa nchini wakidai kuwa Dulla Mbabe alichapwa.

Promota wa pambano hilo, Jay Msangi alisema pambano hilo limeshapata wadhamini wa kulipiga tafu na kwamba wanatarajia kuona pambano lenye upinzani mkubwa wa jadi baina ya mabondia hao ambao wamekuwa wakiwindana muda mrefu.

“Tunatarajia kuwa na mapambano mengi ya utangulizi ambayo yatashirikisha mabondia wenye vipaji wa hapa hapa nchini,” alisema Msangi.

Mwakilishi wa GSM, mmoja wa wadhamini, Badram Abubakar alisema wameingia katika ngumi kutokana na ukweli kuwa mchezo huo ni wa pili baada ya soka kwa kuwa na mashabiki wengi hapa nchini.

Alisema kuwa chapa yao ya Anta Sport inajishughulisha na masuala ya michezo na mmoja wa mabalozi wake ni bondia maarufu duniani, Manny Pacquiao wa Ufilipino.

Advertisement

“Tupo katika michezo muda na mbali ya kudhamini Yanga, tumeamua kupanua wigo kwa kuingia katika ngumi, mchezo ambao unapendwa sana nchini baada ya soka,” alisema Abubakar.

Alisema kuwa mbali ya soka na ngumi, pia wanadhamini mpira wa kikapu kupitia chapa yao ya Anta Sports ambao wao ndiyo mawakala wakuu wa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.

Katibu Mkuu wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa nchini, TPBRC Yahya Poli alisema  kuwa wamelipitisha pambano hilo huku wakiomba wadhamini kujitokeza kwa wingi kudhamini pambano hili.

Advertisement