Duh! Hii bei anayouzwa Eriksen Spurs noma mazee

Muktasari:

  • Eriksen alikuwa kwenye rada za Zidane katika awamu yake ya kwanza alipokuwa kocha wa Real Madrid kati ya mwaka 2016 na 2018 na ripoti zinadai wababe hao wa Hispania huenda wakapeleka mzigo huko Spurs mwishoni mwa msimu huu kupata saini ya mchezaji huyo.

LONDON, ENGLAND.TOTTENHAM Hotspur imeiambia Real Madrid itapaswa kuvunja rekodi ya uhamisho kama kweli inahitaji kupata saini ya kiungo fundi wa mpira, Christian Eriksen.

Staa huyo wa kimataifa wa Denmark anatajwa kurudi kwenye mipango ya Real Madrid akidaiwa huenda akanaswa kwenye dirisha lijalo la msimu hasa baada ya wababe hao wa Bernabeu kumrudisha Zinedine Zidane kwenye benchi la ufundi.

Eriksen alikuwa kwenye rada za Zidane katika awamu yake ya kwanza alipokuwa kocha wa Real Madrid kati ya mwaka 2016 na 2018 na ripoti zinadai wababe hao wa Hispania huenda wakapeleka mzigo huko Spurs mwishoni mwa msimu huu kupata saini ya mchezaji huyo.

Licha ya kwamba kiungo huyo kuripotiwa kukataa ofa tatu za kuongeza mkataba mpya Spurs na kufanya mkataba wake wa sasa kubakiza miezi 15 tu kabla ya kufika tamati, Spurs bado inaamini mchezaji huyo ana thamani ya Pauni 200 milioni.

Kwa maana hiyo, Real Madrid sasa itabidi ilipe pesa inayozidi ile Pauni 198 milioni iliyolipwa na Paris Saint-Germain kupata saini ya Neymar kutoka Barcelona, Agosti 2017.

Barcelona nayo imeonyesha dhamira ya kumtaka Eriksen, lakini zao hilo la kutoka kwenye akademia ya Ajax litakachofikiria ni kwenda zake Real Madrid tu.