Duh! Eti straika wa Simba ni mnazi wa kulia Yanga!

Muktasari:

  • Mshambuliaji wa Arusha United, Zahoro Pazzi amefunguka na kusema, awali alikuwa shabiki wa kulia wa Yanga na mapenzi hayo yalizimwa baada ya kujiunga na Simba.

 

Dar es Salaam. Hii kitu haikai kichwani hata kidogo, unajua alichokisema mshambuliaji wa zamani wa Simba ambaye kwa sasa anakipiga Klabu ya Arusha United, Zahoro Pazzi.

Katika historia ya maisha yake ya soka, awali alikuwa mnazi wa kulia wa Yanga, lakini alibadili msimamo wake baada ya Simba kumsajili.

Pazzi ambaye baba yake mzazi ni mlinda mlango na kocha wa makipa wa zamani wa Simba amelisimualia MCL Digital namna ilivyokuwa hadi akamaliza.

Anasema, alikuwa mpenzi wa jezi za njano na kusababisha roho yake ilikuwa haitulii pindi anapowaona mashabiki wa Yanga mtaani kwao, jambo lililomfanya hata akawa anapiga hodi na kuomba nguo hizo ili afurahishe nafsi yake.

Anasema, kipindi hicho alikuwa hana uwezo wa kununua kitendo ambacho kilimuuma mzee wake, Idd Pazzi akashawishika kufanya kazi ya ziada ya kumtafutia jezi za Yanga mtoto wake huyo ili amfurahishe.

Lakini, mapenzi hayo yalibadilika baada ya Simba kumsajili na kuanza kuichezea timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi.

"Huwezi kuamini na sijawahi kumwambia mtu mwingine yeyote ndiyo leo nakutamkia wewe, kuwa historia yangu nilipokuwa mtoto nilikuwa Yanga kwa kulia, lakini, mazingira ya kazi ndiyo yalinibadilisha na kuingia Simba,"alisema Zahoro aliyesajiliwa Mtibwa Sugar msimu wa 2008-2009 akitokea Sekondari ya Makongo.

Alipoulizwa akiwa na Simba, mapenzi yake yalikuwa bado Yanga na alicheza vipi?

Pazzi anasema: "Sikujali hilo. Nikiwa na Simba nilicheza kwa mapenzi yangu yote kwa Simba, sikuangalia hilo na taratibu, nikajikuta hata msimamo wangu unakuwa wa kisimba na Yanga ikabaki historia tu."

"Kama unavyojua mimi ni mchezaji, kazi yangu ni mpira siangalii mapenzi yangu ni nini, nakuwa mtu wa kufanya kazi kwa sababu ndiyo inanifanya nitambe mjini,"alifafanua mchezaji huyo mwenye uwezo wa kupiga mashuti ya mbali.

Pazzi ameongeza hata sasa, akiitwa kuichezea Simba kwa mara nyingi au Yanga ni kwa ajili ya kazi tu na si vingine.