Duh! Coutinho, Busquets washushiwa jumba bovu

Muktasari:

Coutinho amekuwa akihusishwa na Chelsea, lakini mashabiki wa timu hiyo wameiambia klabu yao isimsajili baada ya kiwango cha hovyo.

HABARI ndiyo hiyo. Philippe Coutinho, Sergio Busquets na Jordi Alba wameripotiwa kwamba huenda wakapigwa panga huko kwenye kikosi cha Barcelona baada ya kucheza hovyo dhidi ya Liverpool na kuigharimu timu hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kocha Ernesto Valverde naye yupo kwenye mashaka makubwa ya kuhusu usalama wa ajira yake huko Nou Camp baada ya kikosi hicho kupoteza uongozi wake wa mabao 3-0 na kuchapwa 4-0 huko Anfield katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa mujibu wa AS, kuna mastaa watatu ambao wapo kwenye hatari ya kuondolewa kwenye kikosi kutokana kipigo hicho cha aibu.
Coutinho ameshindwa kuonyesha makali kwenye mechi hiyo iliyomshuhudia akirudi Anfield na hakumaliza mechi hiyo. Amekuwa akihusishwa na Chelsea, lakini mashabiki wa timu hiyo wameiambia klabu yao isimsajili baada ya kiwango cha hovyo. Coutinho ameshindwa kucheza kwenye ubora wake tangu alipotua Nou Camp Januari mwaka jana kwa ada ya Pauni 145 milioni.
Kuhusu Busquets, ambaye yupo kwenye timu hiyo kwa miaka 11, huenda naye akakumbana na panga sawa na kinachodaiwa kwamba kitamkuta Alba. Baada ya mechi, Busquets aliwaomba radhi mashabiki wa Barcelona kwa kile kilichotokea AS Roma msimu uliopita na huko Liverpool msimu huu kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.