Drogba astaafu soka akiacha ujumbe mzito

Muktasari:

Drogba ametangaza uamuzi huo kupitia ukurasa wake wa Istagram jana Jumatano jioni akisema anajivunia mafanikio makubwa aliyopata tangu aanze kulisakata soka. Nyota huyo raia wa Ivory Coast ametangaza kustaafu soka akiwa na miaka 40, na ameshatupia wavuni amabao 164 kwenye michezo yote akiwa Stamford Brigde.

Mshambuliaji wa zamani wa Chelsea, Didier Drogba ametangaza kustaafu soka kuanzia jana Jumatano jioni. Muivory Coast huyo ameondoka kwenye ulingo wa soka akiwa ameshatwaa mataji mbalimbali ambayo kwake anajisikia ni fahari kubwa.

Drogba alitangaza uamuzi huo kupitia ukurasa wake wa Istagram jana Jumatano jioni akisema anajivunia mafanikio makubwa aliyopata tangu aanze kulisakata soka.

Nyota huyo raia wa Ivory Coast ametangaza kustaafu soka akiwa na miaka 40, na ameshatupia wavuni amabao 164 kwenye michezo yote akiwa Stamford Brigde.

Drogba anaondoka kwenye soka akiwa ametwaa mataji manne ya Ligi Kuu England, na taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2012 pamoja pamoja na Kombe la FA mara nne, huku Kombe la Ligi akinyakua taji hilo mara tatu.

Baada ya kuondoka Chelsea, Drogba alikwenda nchini Marekani ambako alikuwa akiichezea klabu ya Phoenix Rising ambayo yeye pia ni miongoni wa wamiliki wake.

Nyota huyo anatarajiwa kutundika daruga mwishoni mwa mwezi huu wakati wa finali ya Kombe la Ligi ambapo timu yake itacheza dhidi ya Louisville City.

Drogba amedumu kwa miaka 20 kwenye soka ambapo amesema kwa mafanikio aliyopata hana budi kujivunia katika safari yake ambayo imempa mafanikio lukuki.

“Mtu akikusifikia kwamba una na malengo mazuri na makubwa, wewe sema nashukuru na ongeza juhudi na ufanisi ili yawe katika uhalisia”

Aliongeza kuwa, “Napenda kuwashukuru wachezaji wote, makocha, timu mbalimbali na mashabiki kwa kufanikisha safari yangu kwa kila namna ya kipekee.”

Alisema, “Nawashukuru familia yangu kwa upendo wao kwangu, pia timu yangu kwa kunipa sapoti kipindi chote.”

Drogba aliwahi kuichezea Le Mans na Guingamp kabla ya kujiunga na Marseille ambayo aliachana nayo na kujiunga na Chelsea mwaka 2004 kwa dau la Pauni 24 milioni.

Aliachana na Chelsea kisha kujiunga na Ligi Kuu ya China kwenye klabu ya Shangai Shenshua majira ya kiangazi 2012, lakini miezi sita baadaye alihamia Galatasaray ya nchini Uturuki kabla ya kurejea tena Stamford Bridge mwaka 2014.

Alipoondoka Chelsea alikuwa akiishi Marekani na baadaye akawa akiendelea na shughuli zake huku akiwa klabu ya Phoenix. Pia aliendelea na miradi mingine iliyohusisha shughuli zake akipanua kazi zake hadi barani Afrika. Baadaye alimua kujihusisha na shughuli ya ukocha.