Dortmund yafura Sancho kujirusha

Dortmund, Ujerumani. Borussia Dortmund imekasirishwa na kitendo cha mchezaji wao, Jadon Sancho kwenda kwenye sherehe ya straika Tammy Abraham wakati alisema kwamba anaumwa.

Staa huyo aliyekuwa akisakwa na Manchester United kwa muda wote wa dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi, ambaye kwa sasa yupo kwenye kikosi cha England, alikosekana kwenye mechi ya Dortmund iliposhinda 4-0 dhidi ya Freiburg huku akiripotiwa kuwa mgonjwa.

Na jambo hilo lilimfanya akosekane mazoezini tangu mwanzoni mwa wiki iliyopita. Lakini, ripoti zinadai kwamba Sancho alikuwa mmoja wa mastaa watatu wa England ambao walikwenda kwenye sherehe ya Abraham ya kutimiza miaka 23.

Sancho, Abraham na Ben Chilwell waliokuwa sehemu ya sherehe hiyo ilikuwa na wageni 20 marafiki na wanafamilia.

Wote hao wanatarajia kucheza dhidi ya Wales, Alhamisi hii huku kitendo hicho kikiwaweka kwenye hatari kubwa ya kupigwa chini.

Shuhuda mmoja alisema: “Ilikuwa sherehe nzuri. Tulitaka kufanya kitu kimoja kizuri, lakini hatukujua kile ambacho kingekuja kutokea.”

Sancho kwa muda wote wa dirisha la usajili alikuwa kwenye rada za Man United, ambapo mabosi wa klabu hiyo ya Old Trafford ilisema kwamba watarudi tena Dortmund, Januari kwa ajili ya kunasa huduma ya Mwingereza huyo.