Dortmund, Bayern katika mechi ya ubingwa

Muktasari:

  • Bayern Munich ndio mabingwa wa kihistoria wa taji la Ligi Kuu ya Ujerumani wakiwa wamelinyakua mara 28 huku Dortmund wakibeba mra tano (5)

Dortmund,Ujerumani. Hapana shaka yoyote kwamba mechi ya watani wa Jadi baina ya Borussia Dortmund na Bayern Munich leo saa 1.30 usiku imeshikilia hatima ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani 'Bundesliga' msimu huu.
Mechi hiyo maarufu kama 'Klassiker' itakayochezwa katika uwanja wa nyumbani wa Dortmund, Signal Iduna Park inazikutanisha timu hizo mbili zikiwa katika vita kali ya ubingwa ambayo inaweza kuendelea au kupoa baada ya mchezo wa leo.
Wakiwa nyuma kwa tofauti ya pointi nne (4), wenyeji Dortmund wanalazimika kuibuka na ushindi katika mchezo huo ili waendelee kuweka hai matumaini yao ya kutwaa taji hilo msimu huu ambalo litakuwa la sita kwao.
Dortmund wana pointi 57 na wapinzani wao wana pointi 61 hivyo ushindi katika mchezo wa leo maana yake utawafanya kuongeza presha zaidi kwa Bayern kwenye mbio za kuwania ubingwa.
Lakini kwa Bayern wenyewe mchezo wa leo unaonekana hauna presha kubwa kwao kwani matokeo ya ushindi, sare au hata kufungwa bado yatawafanya waendelee kukaa kileleni.
Hata hivyo ushindi na sare ndio matokeo mazuri zaidi kwa Bayern kwani ama yatawafanya kuongeza pengo la pointi na kufikia saba ikiwa watapa ushindi lakini kama wakitoka sare maana yake watakuwa wamelilinda pengo la pointi nne lililopo sasa.
Matumaini makubwa kwa wenyeji Borussia Dortmund yapo kwa nyota wao mwenye umri wa miaka 19, Erling Haaland ambaye amekuwa hatari katika kufumania nyavu tangu ajiunge na timu hiyo katika dirisha dogo la usajili la Januari, akiifungia Dortmund mabao 10 katika mechi 10 alizoichezea.
Lakini pia watamtegemea zaidi kinda la Kiingereza, Jadon Sancho ambaye ndiye amekuwa injini ya Dortmund katika kuzalisha mabao, msimu huu akifunga 14 na kupiga pasi 17 zilizozaa mabao.
Kwa upande wa Dortmund hapana shaka silaha yao ni kinara wa ufungaji katika Ligi Kuu ya Ujerumani msimu huu, Robert Lewandowski ambaye amewafungia mabao 27 msimu huu katika ligi hiyo.
Uwezo wake wa kufumania nyavu na uzoefu alionao dhidi ya Dortmund ambayo aliwahi kuichezea ni mambo ambayo bila shaka yanaweza kuwapa Bayern hali ya kujiamini katika mchezo huo.
Ukiondoa Lewandowski, nyota mwingine ambaye Bayern wanamtegemea leo ni Serge Gnabry ambaye katika mechi 25 alizoichezea Bayern katika Ligi Kuu msimu huu, amefunga mabao 11 na kupiga pasi 10 zilizozaa mabao.