Dodoma Jiji yaikabili Majimaji kwa tahadhari

Saturday June 27 2020

By Masoud Masasi

Dodoma Jiji FC inaongoza msimamo wa kundi A la Ligi Daraja la Kwanza ikiwa na pointi 42 wakati Majimaji iko nafasi ya tatu ikiwa na pointi 37

Masoud Masasi

Kiungo wa Dodoma Jiji FC, Rajab Mgalula amewasisitiza wachezaji wenzake kucheza kwa tahadhari kubwa dhidi ya Majimaji ugenini leo, kwani mechi hiyo imeshikilia hatima yao ya kupanda Ligi Kuu.

Mgalula alisema mechi hiyo na Majimaji ndio itakuwa ngumu kwao na wanatakiwa kupambana sana kuweza kuondoka na ushindi ambao utawafanya wawe katika nafasi nzuri ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Alisema wamebakiza mechi tatu lakini hiyo ya Majimaji kama wakishinda basi watakuwa na kazi rahisi katika mbili zilizobaki kwenye harakati zao za kuwania kupanda Ligi Kuu.

“Tumebakiza mechi tatu hii ya Majimaji,Mbeya Kwanza na tunamaliza na Iringa United kikubwa hapa tunatakiwa kukomaa sana maana Ihefu wanakuja na kasi kubwa sana hivyo lazima tukimbizane nao.

Advertisement

Huu ndio msimu wetu wa Dodoma kuweza kupanda Ligi Kuu msimu ujao hivyo ni lazima tukomae sana haswa hii mechi na Majimaji ambayo ndio ngumu tukishinda hii basi tutakuwa tumenusa kupanda daraja,” alisema Mgalula.

Alisema mchezo huo utakuwa mgumu kwani Majimaji nao wako katika mbio za kupanda daraja msimu ujao kitu ambacho kitakoleza upinzani kwenye pambano hilo.

“Huu ni mchezo mgumu sana kwetu kwani wapinzani wetu nao wako katika mbio za kupanda daraja tunachotakiwa ni kukomaa na kuweza kupata ushindi katika pambano hili la ugenini,”alisema Beki huyo.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma timu hizo zilitoka sare ya bao  1-1.

 

 

Advertisement