Djuma aibua mapya Simba ikienda Mtwara

Wednesday September 12 2018

 

By Thobias Sebastian

Dar es Salaam. Msafara wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, klabu ya Simba unaondoka kesho Alhamisi kwenda Mtwara tayari kwa mchezo wao dhidi ya Ndanda FC lakini katika safari hiyo yameibuka mambo makubwa mawili ambayo ni hatari sana.

Simba ambayo mchezo huo utakuwa ni wa tatu kwao katika msimu huu baada ya kuzifunga, Tanzania Prisons na Mbeya City jijini Dar es Salaam.

Na mambo ambayo yameibuka katika safari hiyo, la kwanza ni kwamba, inadaiwa kocha wao msaidizi, Mrundi Masoud Djuma hatasafiri na atabaki Dar es Salaam na pili, watatumia usafiri wa ndege.

Djuma ambaye hivi karibuni kuliibuka taarifa kuwa yuko mbioni kutimuliwa na mabosi wake hao kutokana na sababu mbalimbali taarifa ambazo zilipotelea angani kabla ya hili lingine kuibuka.

Jumla ya wachezaji 20, pamoja na benchi la ufundi litakaloongozwa na Kocha Mkuu Patrick Aussems ndiyo watakaopanda ndege na hii ni mara ya kwanza kwa Simba.

Kwa takribani misimu minne tangu Ndanda ilipopanda Wekundu wa Msimbazi hao walikuwa wakitumia usafiri wa basi.

Baki na Djumba, benchi la ufundi la Simba, litakuwa na mapungufu baada ya meneja wao, Richard Robart kufungiwa mwanzoni mwa wiki hii  kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Mchezo wa Simba na Ndanda utapigwa  Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Advertisement