Djuma aanza kibarua rasmi AS Kigali leo

Muktasari:

Kocha Masoud Djuma, leo ameanza rasmi kukifundisha kikosi chake kipya cha AS Kigali ambacho kinashiriki ligi kuu ya Rwanda, jana Djuma alishuhudia timu yake ikitoka suluhu.

Dar es Salaam.Aliyekuwa kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma ameanza kazi rasmi leo Jumatatu kukinoa kikosi chake kipya cha AS Kigali inayoshiriki Ligi Kuu Rwanda.

Djuma raia wa Burundi jana Jumapili aliishuhudia timu yake ikicheza mechi ya ligi na kutoka suluhu.

Akizungumza na Mwanaspoti Online, Djuma alisema anaamini atapewa ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wachezaji na uongozi wa timu hiyo.

"Leo ndiyo nimeanza kazi rasmi ya kufundisha ingawa jana (Jumapili) nilishuhudia timu yangu ikicheza mchezo wa ligi. Kikosi ni kizuri na tutafanya vizuri.

"Ligi ndiyo kwanza inaanza kama kitakuwa na marekebisho basi ni hapo baadaye ila kila kitu kinakwenda vizuri," alisema Djuma

Djuma ambaye amesaini mkataba wa mwaka mmoja aliondoka Simba baada ya kukubaliana kuvunja mkataba wake wa mwaka mmoja kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kushindwa kuelewana na kocha mkuu Mbelgiji, Patrick Aussems.