Diouf aipa Kombe Misri

Muktasari:

  • Historia inaonyesha kuwa Misri ndiyo timu iliyotwaa mara nyingi ubingwa wa AFCON pindi ikiwa mwenyeji ambapo katika awamu nne ambazo walikuwa wenyeji, imefanya hivyo mara tatu mwaka 1959, 1986 na 2006 huku ikilikosa mara moja amwaka 1974.

NYOTA wa zamani wa Senegal na Liverpool, El Hadji Diouf ameitabiria mema timu ya Taifa ya Misri kwa kuipa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika nchini humo mwezi ujao.

Diouf ambaye alikuwemo kwenye kikosi cha Senegal kilichocheza fainali ya AFCON mwaka 2002 na kufungwa na Cameroon kwa penati 3-2 baada ya kutoka sare tasa ndani ya muda wa kawaida, anaamini kuwa faida ya uenyeji itawabeba Misri mbele ya timu nyingine shiriki kwenye mashindano hayo.

“Mtazamo wangu Mashindano ya Mataifa ya Afrika ni kwamba safari hii yatakuwa magumu kwa kila timu kwa sababu yanashirikisha nchi nyingi na kila moja inafahamu kuwa Misri inapoandaa mashindano mara nyingi imekuwa ikitwaa taji kwa sababu wanakuwa na timu imara wawapo nyumbani na wamekuwa wakizipa presha timu nyingine.

“Pindi Misri wanapoandaa mashindano, ni vigumu kombe kuchukuliwa nje ya ardhi yao. Nadhani itakuwa ni kazi ngumu kuifunga Misri pale inapokuwa nyumbani,” alisema Diouf.

Pamoja na kuwapigia chapuo wenyeji, Diouf anaamini nchi yake Senegal ndiyo timu pekee inayoweza kutoa ushindani na ikiwezekana kuchukua ubingwa mbele ya Misri kutokana na ubora wa kikosi chake.

Historia inaonyesha kuwa Misri ndiyo timu iliyotwaa mara nyingi ubingwa wa AFCON pindi ikiwa mwenyeji ambapo katika awamu nne ambazo walikuwa wenyeji, imefanya hivyo mara tatu mwaka 1959, 1986 na 2006 huku ikilikosa mara moja amwaka 1974.

Mwaka huo 1974, ubingwa ulichukuliwa na Zaire ambayo kwa sasa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).