Dilunga kula sahani moja na Makambo

Muktasari:

Dilunga ana mabao 10, moja pungufu na yale ya Makambo, ambapo alisema kauli mbiu yake kwa msimu huu ni kiatu kwenda kwa mzawa, kitendo cha Makambo kuwa juu yake alidai kinampa morali ya kujituma kwa bidii ili kufunga kila mechi.

STRAIKA wa Ruvu Shooting, Said Dilunga anashika nafasi ya pili katika orodha ya Wafungaji mabao wa Ligi Kuu Bara, huku akifunguka wazi akili yake ni kuhakikisha anakula sahani moja na mfungaji wa Yanga, Heritier Makambo mwenye mabao 11.

Dilunga ana mabao 10, moja pungufu na yale ya Makambo, ambapo alisema kauli mbiu yake kwa msimu huu ni kiatu kwenda kwa mzawa, kitendo cha Makambo kuwa juu yake alidai kinampa morali ya kujituma kwa bidii ili kufunga kila mechi.

“Wazawa lazima tuamke kupambana ili kurejesha heshima waliyokuwa nayo mastraika wa zamani walioacha rekodi zao kwenye ligi kuu Bara na nyingine bado hazijavunjwa kama ya Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ mwenye mabao 26.

“Tukianza kuonyesha makali yetu hata tahamani zetu zitapanda kama wanavyochukuliwa wageni, naamini inawezakana mzawa msimu huu akatwaa kiatu cha dhahabu kwani Makambo, Okwi na Kagere naona wa kawaida ila wanajuhudi na dhamira ya kutimiza malengo yao.”

Said Khamis wa Mbao FC anamiliki mabao sita alisema kinachotakiwa kufanyika kwa wazawa ni kubadilika na kuamua kuwa na malengo ya kufanya kitu cha kimapinduzi kwenye ligi kuu, akitolea mfano wa kutunza viwango vya kuwa juu muda wote.

“Kwanza lazima tujitoe kikamilifu kujua soka ni kazi tulioichagua kwa ajili ya kutengeza uchumi wetu, mbali na hilo ni kazi yenye heshima kubwa duniani, tukijua tunafuatiliwa na watu wa kila aina tutalazimika kubadili mtindo wa maisha kwa maana ya kujituma kwa bidii.