Dili la Sancho, Jurgen Klopp atamnyoosha Ole kweupe

MANCHESTER, ENGLAND. OLE Gunnar Solskjaer imekula kwake. Kitendo cha kuruhusu mabosi wa Manchester United kushindwa kunasa huduma ya Jadon Sancho katika dirisha la majira ya kiangazi la mwaka huu, kitamgharimu kwa kiwango kikubwa katika mpango wa kupata saini ya Mwingereza huyo.

Man United ilipewa nafasi kubwa ya kunasa saini ya Sancho na hata wenyewe walikuwa na uhakika kwamba winga huyo wa Borussia Dortmund angekuwa mchezaji wao kabla ya dirisha la usajili halijafungwa Jumatatu iliyopita. Lakini, dili hilo limeshindwa kutimia.

Man United iliamini Dortmund watashusha bei wanayomuuza staa huyo, Pauni 108 milioni baada ya kugomea ile Agosti 10 ambayo ilikuwa siku ya mwisho waliyowapangia wababe hao wa Ligi Kuu England kwamba wawe wamekamilisha usajili huo. Lakini, baada ya Agosti 10 kupita Dortmund ni kama ilikuwa imefunga milango ya kumuuza winga huyo wa kimataifa wa England.

Solskjaer alipewa nafasi kubwa ya kumnasa Sancho mwaka huu kwa sababu timu yake ilikuwa na pesa ya kutosha kufanya hivyo.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp mara nyingi amekuwa akizungumza juu ya kuhitaji huduma ya mchezaji huyo, lakini kwenye dirisha la usajili wa majira ya kiangazi mwaka huu hakuwa na pesa za kutosha kunasa saini yake. Hakuwa na uwezo wa kumnunua Sancho kabla ya kuuza mastaa wengine.

Janga la corona limeziathiri klabu nyingi kiuchumi, hivyo Liverpool hawakuwa na uwezo wa kuwa na Pauni 108 milioni ambazo zilikuwa zikihitajika na Dortmund.

Klopp aliulizwa kuhusu Sancho na amekiri: “Sidhani kama usajili wake ungewezekana msimu huu.”

Na baada ya hapo, aliongeza: “Jezi nyekundu ya Liverpool itamfaa zaidi.”

Jambo hilo linawafanya Man United kuwa kwenye wakati mgumu katika mpango wa kunasa saini ya Sancho. Bila shaka kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi la mwakani, Man United itapata upinzani mkali kutoka Liverpool kufukuzia huduma ya Sancho, ambaye pia atakuwa na wigo mpana wa kuamua ni wapi aende wakati atakapoamua kurudi England.

Na wachambuzi wa mambo ya soka wanadai kwamba litakapokuja suala la kunasa saini ya Sancho, Klopp atakuwa na nafasi kubwa kuliko Solskjaer.

Kwa mujibu wa The Independent, Sancho kushindwa kwenda Man United mwaka huu kutamfanya kuanza kutafakari upya hatima yake na huenda akaamua kwenda Liverpool au Bayern Munich na hapo Man United itakuwa imekula kwao. Hata hivyo, kwa mujibu wa Manchester Evening News, Man United imemworodhesha Sancho kwenye orodha ya wachezaji itakaotaka saini zao wakati dirisha la Januari litakapofunguliwa.

Mabosi wa Old Trafford wanaamini kwamba wakisubiri msimu umalizike, basi mambo yatakuwa mazito kwa sababu ukiziweka kando Bayern Munich na Liverpool, Real Madrid nao wataingia kwenye mbio.

Sancho amefunga mara moja na kuasisti mara mbili katika mechi alizochezea Dortmundi msimu huu, wakati msimu uliopita alikuwa moto alipofunga mabao 20 na kuasisti mara 20 katika michuano yote aliyocheza.