Dili la Lukaku Inter lipo hivi

Muktasari:

Kocha wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer anatafuta mabeki wa kuja kuimarisha safu yake ya ulinzi na hivyo anamtazama Skriniar kuwa ni mtu mwafaka kama atapatikana.

MILAN, ITALIA.HAIWEZEKANI. Inter Milan wamegomea sharti la Manchester United la kuwataka wamjumuishe beki wa kati Milan Skriniar kwa ofa yao ya kumsajili straika Romelu Lukaku.
Lukaku amekuwa akiwindwa na Inter Milan tangu ilipoanza kuwa chini ya kocha Antonio Conte na straika huyo wa Kibelgiji mwenyewe yupo tayari kwenda kukipiga huko San Siro kama Man United watakubali kumpiga bei.
Kuna taarifa za kutoka Italia zinadai kwamba Lukaku ameshafikia makubaliano binafsi na Inter Milan, ambapo atakuwa akilipwa bonasi ya Pauni 6 milioni, huku kilichobaki ni makubaliano ya klabu pekee. Man United wameripotiwa kuhitaji walau Pauni 60 milioni kwenye mauzo ya mchezaji huyo, huku wakimtaka pia beki wa kati, Skriniar.
Kocha wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer anatafuta mabeki wa kuja kuimarisha safu yake ya ulinzi na hivyo anamtazama Skriniar kuwa ni mtu mwafaka kama atapatikana.
Lakini, Inter wameripotiwa kugomea jambo hilo kwa sababu beki wao huyo wa kati ni mtu muhimu kwenye mipango ya kocha Conte kwa ajili ya msimu ujao.
Skriniar alicheza mechi 46 kwenye kikosi cha Inter Milan kwa msimu uliopita, ikiwamo mechi 35 kwenye Serie A, ambapo timu hiyo ilimaliza kwenye nafasi ya nne. Skriniar alijiunga na Inter akitokea Sampdoria mwaka 2017, alisaini mkataba wa miaka minne wa kubaki kwenye timu hiyo mwezi uliopita.
Kuhusu Lukaku na dili la kwenda Inter, mwenyewe alisema hivi: "Mimi ni shabiki mkubwa wa Serie A. Wale waliokaribu na mimi wanafahamu hilo kwamba siku zote nimekuwa nikitaka kucheza kwenye ligi ya England na Italia. Naipenda Italia.
"Usajili wa (Cristiano) Ronaldo umefanikisha hilo, ligi ya Italia imerudi kama zamani. Sasa Antonio Conte ametua Inter Milan, kitu ambacho ni muhimu, kwangu mimi ni kocha bora duniani."