Dili la Fernandez limekwama hapa tu

Muktasari:

Sporting wanataka kumuuza staa wao huyo kwa pesa inayokaribia Pauni 60 milioni, hivyo kulipwa nusu na kisha nusu nyingine isubiri mafanikio ya uwanjani wanadhani ni kitu kitakachokuwa kigumu kutimia.

LISBON, URENO . MASHABIKI wa Manchester United wanasubiri kwa hamu kukamilika kwa dili la kiungo Bruno Fernandes, lakini unaambiwa hivi bonasi ndiyo inayochelewesha dili hilo kukamilika hadi sasa.

Kiungo huyo fundi wa mpira, Fernandes, 25, alicheza mchezo wa juzi Ijumaa wakati chama lake la Sporting Lisbon lilipomenyana na Benfica na mashabiki wake wanaamini huo pengine ndiyo ulikuwa mchezo wa mwisho kwake kuvaa jezi za timu yao.

Man United wanajaribu kupambana kunasa huduma ya kiungo huyo na itawashuhudia wakiilipa Sporting Pauni 34 milioni na Pauni 25.5 milioni zitakazolipwa kama bonasi kutokana na mafanikio yake ya uwanjani na hapo ndipo kwenye tatizo.

Sporting wanataka kumuuza staa wao huyo kwa pesa inayokaribia Pauni 60 milioni, hivyo kulipwa nusu na kisha nusu nyingine isubiri mafanikio ya uwanjani wanadhani ni kitu kitakachokuwa kigumu kutimia.

Miongoni mwa mafanikio hayo ni kama Man United itashinda ubingwa wa Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Bonasi nyingine iliyowekwa na makamu mwenyekiti mtendaji wa Man United, Ed Woodward kwenye mkataba huo ni kama Fernandes atashinda Ballon d’Or. Sporting wanahofu Man United wapo mbali sana na kufikia mafanikio hayo, hivyo wanataka walipwe mkwanja wao wote kwa sasa wamalizane tu.

Lakini, Man United imegundua Sporting ina shida ya pesa, hivyo wanajaribu kuwalalia ili kumnasa kiungo huyo kwa pesa ndogo na si Pauni 60 milioni wanazotaka Wareno hao. Staa Fernandes akitua Old Trafford atakwenda kulipwa mshahara wa Pauni 120,000 kwa wiki.